Mkuu wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya,   Reuben Mfune akifungua mafunzo hayo ya kimataifa ya kujengea uwezo wataalamu wa Tathimini ya Maji kwa  Mazingira, Pembeni yake ni Mkuu wa Mradi wa wa Utafiti wa  EFLOWS Prof. Japhet Kashaigili kutoka SUA.
 Mtafiti Mkuu wa Mradi huo kutoka (SUA) Prof. Japhet Kashaigili akieleza malengo ya Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wataalam wa masuala ya Maji kwa Mazingira na tathimini yake kutoka nchi nzima na nchi zingine 11 za magharibi mwa bahari ya Hindi.
Meneja wa Programu ya Mazingira ya Bahari (WIOMSA) ambao ndio wafadhili wa mafunzo hayo, Dk Mathias Igulu akitoa salamu za Taasisi yao umuhimu wa mafunzo hayo kwa nchi wanachama.
Mratibu wa Mradi wa Tathimini ya maji kwa mazingira EFLOWS Dk. Winfred Mbungu akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi mara baada ya kufungua mafunzo hayo ya siku tano.
  Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka Taasisi mbalimbali nchi nzima ambazo zinahusiana na Sekta ya Maji,Mazingira,Misitu na Kilimo.
 Washiriki wa ma mafunzo hayo wakifuatilia hotuba za ufunguzi na uwasilishwaji wa mada mbalimbali kwenye mkutano huo Wilayani Mbarali.
Mafunzo yakiendelea.
 Washiriki wa ma mafunzo hayo wakifuatilia hotuba za ufunguzi na uwasilishwaji wa mada mbalimbali kwenye mkutano huo Wilayani Mbarali.
Mafunzo yakiendelea.
Mafunzo yakiendelea.
 Washiriki wa ma mafunzo hayo wakifuatilia hotuba za ufunguzi na uwasilishwaji wa mada mbalimbali kwenye mkutano huo Wilayani Mbarali.
Mafunzo yakiendelea.


Na Amina Hezron, Mbarali
 

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia ufadhili wa Taasisi inayojishughulisha na tafiti za utunzaji wa Bahari (WIOMSA) wameendesha mafunzo ya Kimataifa ya kuwajengea uwezo Wanasayansi, Mameneja na wadau wengine namna ya kuendesha na kufanya tathimini ya Maji kwa Mazingira katika ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi.

Akifungua mafunzo hayo jana Septemba 19, 2022 Wilayani Mbarali mkoani Mbeya, Mkuu wa Wilaya hiyo Reuben Mfune amewataka wadau waliopata mafunzo hayo kuhakikisha wanakwenda kuyafanyia kazi na kuwafundisha wengine kwenye ofisi wanazotoka ili kutimiza malengo ya mafunzo hayo ambayo yanataka kuwepo na utiririkaji wa maji safi na salama kwenye mito kuelekea baharini mwaka mzima.

 “Wale ambao wako ukanda wa juu ya mto unakoanzia wanatakiwa kujua fika shughuli za uharibifu wanazozifanya kule ndizo zinazoleta athari kwenye mabwawa ambayo yanajaa tope ambalo linakwenda mpaka Baharini na kuaathiri viumbe vilivyomo katika Mito, Maziwa na Bahari”, alisema Mfune.

Mfune amewapongeza SUA na WIOMSA kwa kuandaa mafunzo hayo  kwakuwa yanaendana na kazi inayoendelea ya kurejesha afya ya Mito na kupunguza madhara yanayotokana na uchafuzi wa Mazingira katika mito, kwani ni jambo jema kufanyika na litakuwa msaada mkubwa kwa Taifa.

Aidha alisema zipo shughuli nyingi za kibinadamu zinazofanywa kwenye vyanzo vya maji na kandokando ya mito kama vile ukataji miti hivyo,ufugaji usionzingatia ukubwa wa eneo hivyo amewataka Wananchi kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na serikali katika kusimamia sheria na kanuni zilizowekwa ili kuhifadhi mito na mazingira kwa faida ya kizazi hiki na kijacho.

“Maji haya yana umuhimu kwa taifa zima kama bwawa la Nyerere ambalo linajengwa kwa gharama kubwa. Iwapo litashindwa kufanya kazi kutokana na ukosefu wa maji maana yake serikali itakuwa imepoteza fedha hizo bure, lakini pia tuna bwawa la umeme la Mtera na  Kidatu haya yote yasipoweza kufanya kazi tutakuwa tunapunguza uwezo wa kuwa na Tanzania ya viwanda”, alisema Mfune.

Aidha amewataka wadau wengine kuendelea kujitokeza kusadia jitihada za Serikali na wadau waliopo sasa ili kuhakikisha Mito inaendelea kutiririka mwaka mzima na hivyo kuwataka Wananchi kuheshimu Sheria zilizowekwa kwakuwa zipo kwa manufaa ya watanzania wote.

Akizungumzia mafunzo hayo Mtafiti Mkuu wa Mradi huo kutoka (SUA) Prof. Japhet Kashaigili alisema lengo kubwa la mafunzo hayo ni kujenga Wataalamu na utaalamu wa kuweza kufanya tathimini ya maji kwa mazingira ili kusaidia wanapofanya maamuzi katika kugawana maji iwe kwa ajili ya maendeleo endelevu.

“Ni mafunzo ya kujenga uwezo ambayo yana vitendo ndani yake. wataona shughuLi zinazofanyika kama sehemu ya kuhifadhi mazingira na kilichopelekea shughuLi hizo zifanyike pamoja na sababu za msingi za kuwezesha kwanini hiyo tathimini ya maji kwa mazingira ifanyike na shughuli gani zifanyike kwenye maeneo hayo. Hivyo mahari kwingine watafanya wao wenyewe kama sehemu ya mazoezi”, alisema Prof. Kashaigili.

Prof. Kashaigili amefafanua kuwa tathimini hiyo ya maji kwa mazingira itawezesha kuhusanisha madhara yanayotokana na shughuli mbalimbali zinazozifanywa na kwa kiasi gani zinapelekea kuathiri  Ukanda wote wa Bahari  ili kuweza kujua chanzo cha tatizo, hatua  tatizo lilipofikia, madhara na namna ya kutatua.

“Hii itasaidia nchi kutekeleza Sera ya maji pamoja na Sheria ya maji ya mwaka 2009 ambayo imeainisha katika kugawana maji kwa vipaumbele ni kwa ajili ya matumizi ya Binadamu, Mazingira na kwa shughuli nyingine, hivyo maji kwaajili ya mazingira ilikuwa ni sehemu ambayo haina utaalamu na hakukuwa na jinsi ya kufanya hivyo bila kujenga utaalamu sasa utaalamu upo hivyo ni lazima tujenge sasa Wataalamu wengi “, alisema Prof. Kashaigili.

Meneja wa Programu ya Mazingira ya Bahari (WIOMSA) ambao ndio wafadhili wa mafunzo hayo, Dk. Mathias Igulu amesema kuwa kuna mahusiano makubwa kati ya Bahari na Mito, lakini jambo hilo halijaongelewa sana ndio maana WIOMSA wameona ni vyema kuanzisha mjadala na kuwaleta pamoja Wanasayansi na wadau wengine  kwa maslahi mapana ya uhifadhi wa Bahari, Mito na Mazingira.

“Kwa kushirikiana na chuo chetu kikubwa cha SUA ambacho wote tunajua wana Wataalamu wabobevu kwenye maswala ya Sayansi za Kilimo, Maji na Mazingira, Ufugaji wa Samaki na Sayansi zingine zinazoendana na hizo tumeona ni muda muafaka kushirikiana nao kuwaleta pamoja wadau muhimu nchini na nje ya Tanzania kwa kuwa wanao uwezo mkubwa wa kusimamia” alisema Dk. Igulu.

Ameongeza kuwa maswala ya Bahari na mito ni mambo yanayogusa maisha ya watu kila siku na ni swala la kiusalama pia maana jamii inahitaji kutumia maji katika kuzalisha, hivyo ni jambo muhimu na lazima liangaliwe kwa umakini kwa faida ya nchi zote zinazoguswa na mambo haya.

Alisema, wataalamu wa mambo hayo ya tathimini ya maji kwa mazingira ni wachache sana nchini na hii ni kutokana na kutokuwa na chuo kinachotoa Wataalamu mahususi kwa fani hiyo na hivyo amekiomba Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kuona umuhimu wa kuanzisha mitaala ya masuala ya tathimini ya maji kwa mazingira kwakuwa wanao uwezo na Wataalamu wabobevu.

Akizungumza mmoja ya washiriki wa mafunzo hayo, Mtafiti Msaidizi kutoka Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi (TAFIRI) Wendo Lukwambe alisema mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwao kwakuwa yatawasaidia kujua jinsi mtiririko wa maji unavyoenda na namna ya kutunza maji kwa mazingira kwakuwa isipofanyika hivyo itasababisha kuathirika kwa maji hayo.

“Tunajitahidi sana tujue mawazo na teknolojia za mtiririko wa maji na mazingira kwasababu zitatusaidia hata katika mambo ya samaki kwenye uvuvi. Kuna baadhi ya samaki huwa wanapotea kutokana na mazingira jinsi yalivyobadilika ukija kuangalia chanzo utakuta kinatoka kwenye Maji na Mazingira, hivyo kama tukitunza chanzo cha Maji vizuri kinaweza kutusaidia hata sisi kwenye Bahari na Samaki pia kwa kuepusha vifo na kutoweka kwa aina za samaki”, alisema Lukwamba.

Mafunzo hayo ya siku tano yamewahusisha washiriki kutoka Taasisi mbalimbali za Utafiti katika sekta za Maji, Mazingira, Misitu  na washiriki wengine kutoka nchi za ukanda wa magharibi mwa Bahari ya Hindi ikiwemo  Afrika Kusini, Kenya, Mauritius, Msumbiji, Visiwa vya Shelisheli, Somalia, , Visiwa vya  Comoro, Madagasca na Visiwa vya Reunion ambao wameshiriki kwa njia ya Mtandao (Zoom).

 

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: