MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela amepiga marufuku ufugaji holela ndani ya mji wa Geita na kuiagiza Halmashauri ya Mji huo kuwekea mkazo na kusimamia kanuni za mazingira maeneo ya mjini kwa wanaokiuka.

Shigela ametoa maelekezo hayo alipozungumza na wananchi na viongozi wa mji wa Geita, waliojitokeza kushiriki uzinduzi wa kampeni ya mkoa ya upandaji miti kukabiliana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Amesema ufugaji holela katikati ya mji inasababisha uchafuzi wa mji na kurudisha nyuma juhudi za halmashauri hiyo kukidhi vigezo vya kuwa manispaa, hivyo wanaofanya ufugaji mjini Geita wafuate miongozo kama siyo kuhama.

“Lazima tuheshimu taratibu za kuishi mijini, kama unaona bado unahitaji kufuga ngo’ombe wengi basi maeneo ya wazi ambayo tumetenga kwa ajili ya ufugaji unaruhusiwa kwenda kufanya shughuli za ufugaji siyo katikati ya mji wetu wa Geita.

“Kwa hiyo watendaji wa mitaa, maofisa mifugo, watu wa mazingira, watambueni watu ambao bado wana mifugo mingi katika mji wetu, wapeni angalizo la kuhama, ili waweze kwenda maeneo ambayo tumetenga kwa shughuli za ufugaji,” alisema.

Ameagiza kampeni ya upandaji miti kwenye halmashauri zote mkoani Geita kufanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kupambana kurejesha uoto wa mkoa wa Geita unaozidi kupotea, kutokana na shughuli haramu za binadamu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Profesa Godius Kahyarara ameelekeza wataalamu wa mazingira kufanya tathimini ya maeneo ya kupanda miti, waharibifu wakubwa wa miti na kuhamasisha matumizi ya teknolojia sahihi ya uchimbaji wa madini.

Ofisa Mazingira Mkoa wa Geita, Tito Mlelwa amesema kampeni ya upandaji miti imezinduliwa kwa kupanda miche ya miti 300 mjini Geita na wamejipanga kusimamia usafi wa mazingira na upandaji miti kwenye halmashauri zote mkoani hapa.

Share To:

Post A Comment: