Jeshi la Polisi limeingia katika kashfa nyingine, baada ya askari wake kutuhumiwa kusababisha kifo cha Ulirki Sabas (47), Mkazi wa Kijiji cha Kirongo chini wilayani Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro akiwa mikononi mwao.

Tukio hilo linadaiwa kutokea katika Kituo cha Polisi Usseri wilayani humo ambapo Sabas alikamatwa Septemba 7, mwaka huu, akituhumiwa kushiriki tendo la ndoa na mwanafunzi.

Sabas baada ya kufikishwa kituoni hapo, inadaiwa na Prisila Kavishe (42) ambaye ni mke wake alikuwa buheri wa afya lakini taarifa alizozipata siku mbili mbele za kifo cha mme wake zilimshtua.

Matukio kama hayo kwa Jeshi la Polisi kudaiwa kuhusika kusababisha vifo si ya kwanza kwani yamekuwa yakitokea na kufanyika uchunguzi.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simoni Maigwa, alipozungumza na Mwandishi wetu juzi alisema tayari ameandaa jalada la uchunguzi ili kujiridhisha sababu ya kifo hicho kimesababishwa na nini. “Tunachunguza kujua ukweli na madaktari ndio wanaothibitisha mgonjwa amekufa kwa sababu gani,” alisema Maigwa

Kamanda huyo aliongeza, “tutalichunguza jambo hili kwa uwazi kujua chanzo cha kifo hicho. Mimi siwezi kusema alipigwa au hakupigwa, hivyo tunasubiri majibu ya daktari.”

Akisimulia tukio hilo, Prisila alisema Septemba 7, mwaka huu mumewe alikamatwa na kufikishwa kituo hicho cha polisi kwa madai ya kushiriki tendo la ndoa na mwanafunzi.

Alisema baada ya kufikishwa kituoni hapo, Septemba 6, alimpelekea mumewe chai na kumkuta akiwa mzima wa afya. Baadaye wakajulishwa atafikishwa mahakamani hivyo ndugu wakatakiwa kuondoka kituoni hapo.

Prisila alisema baada ya kurudi nyumbani, jirani yake alimpigia simu anatakiwa kwenda kituo cha polisi kuna tatizo limetokea.

Alisema alipofika kituoni alimkuta mumewe amelazwa chini ya sakafu akiwa hawezi kuzungumza huku akiwa na uvimbe mkubwa kichwani, majeraha mdomoni, jicho moja lilikuwa limeumizwa huku akivuja damu mdomoni.

Alisema alipowauliza askari waliokuwa kituoni nini kimempata mumewe walimjibu alikuwa na kifafa mara alijipiga ukutani jambo ambalo lilimpa shaka.

“Baada ya kuambiwa hivyo nilirudi nyumbani, ilipofika muda wa saa 11 jioni jirani yangu akawa ameniletea simu akanambia ongea na huyu askari, nikapokea ile simu yule askari akanambia njoo haraka hapa kituoni na uje na huyo aliyekuletea simu,” alisema

“Niliongozana naye hadi kituo cha polisi, nilipofika nikakuta mumewangu amelazwa chini barazani pale kituo cha polisi, muda ule alikuwa hawezi kuongea jicho kama limepasuliwa.

“Midomo umevimba na kama vile amevunjwa taya na kwenye utosi kulikuwa na uvimbe mkubwa ambapo alikuwa akivuja damu puani na mdomoni,” alisema

Akisimulia zaidi, alisema,“niliuliza mume wangu amepatwa na nini askari, walitueleza wakati wanataka kumpeleka Ibukoni alitaka kuruka kwenye gari na kwamba walipofika njiani wakawa wamemrudisha kituoni na kumweka mahabusu.”

Mama huyo alisema, “wakaniambia walipomweka mahabusu alijigonga ukutani, askari wale wakawa wananiharakisha mchukueni mtu wenu mpelekeni kituo cha afya Karume ndugu wengine, waliokuwa pale wakambeba kama mtoto na kumpeleka Karume, wale askari wakaniita haraka haraka wakanambia niwape majina yangu nikawapa majina yangu na wakaniambia nisaini.”

“Kuna askari mmoja alikuwa pale mrefu mnene akanambia mnakuja kutuletea mtu wenu mwenye kifafa hapa, niliumia sana kwa majibu yale, nikawa nimetoka nje huyo askari akawa ananifokea akawa anambia njoo hapa wewe mama akanambia haya mfuate mtu wako huko,” alisema na kuongeza:

“Tulienda Karume pale na tulikuwa hatuna Pf3 wala kibali chochote kutoka kituo cha polisi yaani hatukupata msaada wowote wa polisi, madaktari walimwangalia mgonjwa wakatuambia hawamuwezi tumpleke hospitali ya Huruma,” alisema.


Share To:

Post A Comment: