Na Gasto Kwirini wa Jeshi la Polisi


Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema litachukua hatua za kisheria kwa makampuni yote binafsi  ya ulinzi ambayo yanafanya shughuli zake mkoani hapa bila ya kuwa na vibali vya kuendesha makampuni hayo ambavyo vinatolewa na Jeshi la Polisi.


Hayo yamesemwa na Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Mary Kipesha leo Septemba 15, 2022 wakati akizungumza na Uongozi wa Chama kinachosimamia sekta binafsi ya ulinzi Tanzania (TSIA) pamoja na wamiliki  wa makampuni hayo  Mkoa wa Arusha katika kikao kilichofanyika katika bwalo la Maafisa wa Polisi Mkoa wa Arusha.


ACP Kipesha ambaye alimwakilisha kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha alisema kuwa yapo baadhi ya makampuni ambayo yanalinda ofisi, taasisi ama nyumba za watu binafsi lakini hayana vibali vya usajili, hivyo akatoa wito kwa uongozi wa TSIA kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za makampuni yote ambayo yanaendesha shughuli zake bila ya kuwa na vibali ili hatua za kisheria zichukuliwe.


Alisema uwepo wa Makampuni binafsi ya ulinzi umelisaidia Jeshi la Polisi hususani katika suala zima la ulinzi wa raia na mali zao na kubainisha kuwa makampuni hayo yanatoa ulinzi pamoja na kufanya doria maeneo mbalimbali  mkoani hapa  hali ambayo inasaidia kupunguza matukio  ya uhalifu hivyo akawaeleza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kutoa ushirikiano pale unapohitajika.


Afisa huyo mnadhimu wa Polisi alionya tabia ya baadhi ya makampuni kuajiri vijana ambao sio waaminifu  wanaoshirikiana na wahalifu katika maeneo yao ya kazi ama kuajiri wazee  walio na umri zaidi ya miaka 55 na kuwasihi kuajiri vijana ambao wana nguvu na wale waliopitia mafunzo ya Mgambo au JKT.


Sambamba na hilo pia aliwataka viongozi hao kuhakikisha katika malindo yenye silaha, yanakuwa na silaha mbili kwa sababu silaha moja hulinda nyingine hivyo akawataka kuacha tabia ya makampuni  hayo kuweka  silaha moja katika maeneo yao ya ulinzi.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa makampuni ya binafsi ulinzi Tanzania Bwana Felix Kagisa alisema kuwa wamekuja Mkoani Arusha ikiwa ni utaratibu wao wa kawaida wenye lengo la  kusikiliza changamoto mbalimbali wanazozipitia na kutafuta suluhu za  baadhi ya changamoto hizo.


Aliendelea kusema kuwa katika vikao vyao wanautaratibu wa kualika Jeshi la Polisi kwa sababu  sekta hiyo inafanya kazi kwa karibu na Jeshi hilo ambapo alimpongeza Afisa mnadhimu Mkoa wa Arusha kwa mambo mbalimbali aliyowaasa pamoja na kujibu hoja walizoziwasilisha na  wanaamini kupitia kikao hicho changamoto walizoziwasilisha kwake zitatuliwa.

Share To:

Post A Comment: