Mradi wa ujenzi wa maabara changamano awamu ya pili katika Tume ya nguvu za atomu Tanzania ulioanza septemba 16 ,2019 unatarajia kugharimu jumla ya shs 10.4 bilioni hadi kukamilika kwake na unatarajiwa kukamilika septemba 22 ,2022 .
Aidha maabara hiyo ambayo ni ya pili kwa ukubwa Afrika inatekelezwa na mkandarasi Li Jun Development Construction Company Ltd ambapo ujenzi huo umefikia asilimia 97 na kukamilika kwake kutaongeza tija katika utekelezaji wa sera ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia ya mwaka 2013.
Hayo yalisemwa jijini Arusha na Mkurugenzi mkuu wa Tume ya nguvu za atomu Tanzania ,Profesa Lazaro Busagala wakati kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii ilipotembelea Tume hiyo kujionea maendeleo ya mradi huo.
Profesa Busagala alisema kuwa,uwepo wa maabara hiyo utasaidia kuzalisha wataalamu zaidi katika nyama ya teknolojia ya nyuklia ili kusaidia kukuza uchumi kupitia mchango wa teknolojia ya nyuklia katika sekta za afya,kilimo,mifugo,barabara na maji.
"Kupatikana kwa kituo cha mafunzo katika jengo la maabara hiyo kutaongeza wastani hadi kufikia wataalamu 1000 kwa mwaka katika nyanja mbalimbali na kuweza kuimarisha mfumo wa usimamizi wa usalama wa watu na mazingira imara uchimbaji na usafirishaji wa madini ya Urani utakapoanza."alisema .
Profesa Busagala alisema kuwa,maabara hiyo itasaidia sampuli mbalimbali za mazingira na kusaidia kutoa elimu kwa umma ,kwani kwa sasa maabara zilizopo zinaweza kupima jumla ya sampuli za mazingira 800 kwa mwaka na kuwepo kwa maabara hiyo kutasaidia kupima sampuli 3000 za mazingira ambapo matokeo yake yatasaidia kuongeza taarifa za kiusalama za mionzi.
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo Stanslaus Nyongo ambaye pia ni Mbunge wa Maswa Mashariki kuwa, wameridhishwa na ujenzi wa maabara hiyo ambayo imeonyesha uhalisia wa thamani ya fedha zilizotumika huku akipongeza mradi huo kukamilika kwa wakati .
Nyongo alisema kuwa,wamekuwa wakihamasisha na kusimamia matumizi salama ya mionzi katika kuhakikisha watanzania hawaathiriki na mionzi hiyo kwa namna yoyote ile ,hivyo uwepo wa maabara hiyo ni fursa kubwa sana kwani ni maabara ya pili kwa ukubwa Afrika.
Post A Comment: