Moses Mashalla ,Arusha 

Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini,Mrisho Gambo “amechafua hali ya hewa “leo wakati alipotembelea soko la Krokon lililopo jijini Arusha ambapo mbali na kuzungumzia vita anavyopigwa lakini ametamka yuko tayari kuachia nafasi yake ya ubunge kuliko kuungana na mafisadi.

Gambo ametoa kauli hiyo leo wakati alipofanya ziara katika soko hilo ambapo alikabidhi jumla ya mabati 30 na matofali 500 kwa ajili ya ujenzi wa choo cha soko hilo.

Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo Gambo alisema kuwa baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM wamekuwa wakimwita mpinzani lakini potelea mbali yeye ataendelea kupambana na wezi na mafisadi wanaotafuna fedha za umma.

Akiongea kwa jazba katika eneo hilo Gambo alisema kuwa jimbo la Arusha Mjini sio jepesi kama makada wa CCM wanavyodhani bali ni jimbo la watu wanaojielewa kwani wanaweza kuchagua mtu na sio chama.

“Arusha Mjini sio jimbo jepesi hili ni jambo la watu wanaojielewa hapa watu wanaweza kuchagua mtu na sio chama mimi sio mwoga bali nasimamia haki “amesema Gambo 

Gambo amesema kuwa yuko tayari hata kama atadumu kwa miaka mitano kwenye nafasi yake ya ubunge lakini sio kukubaliana na mafisadi na ataendelea kupambana na wanaompiga vita.

“Miaka yangu hii mitano sita comprise na mtu hata nikikaa miaka mitano kama ni gharama ya kupambana na mafisadi sitaogopa kama wananipiga vita wao waendelee “amesisitiza Gambo 

Hatahivyo,amesisitiza kuwa ataendelea kupambana nje na ndani ya chama kupigania maslahi ya wakazi wa jimbo la Arusha Mjini ikiwemo kupambana na rushwa na ufisadi kwa kuwa CCM imekuwa ikipambana na rushwa na ufisadi.

“Bora tuchane mkeka 2025 tukutane kule moto tuliounzisha wa kupambana na rushwa hautasimama hata nikibaki peke yangu nitasema “amesisitiza Gambo 

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Arusha,Hargeney Chitukuro amesema kuwa jiji linachangia kiasi cha sh,1 milioni kuchangia ujenzi huo kama njia ya kumuunga mkono Gambo.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mitumba katika soko hilo,Magreth Mboya amesema kuwa ujenzi wa choo hicho ilikuwa ni ahadi ya mbunge huyo na wanashukuru kwa kutimiza ahadi yake.


Pili Mohammed ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT)kata ya Levolosi amesema kuwa kero ya ukosefu wa choo katika soko hilo ni kero ya muda mrefu na wanashukuru Mbunge kwa kumaliza kero hiyo .


Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: