Waziri wa Maji,Jumaa Aweso ameagiza kuwepo kwa chombo kimoja kitakachosimamia utoaji wa maji katika Mji wa Karatu Mkoani Arusha, kwaajili ya kutoa huduma za maji na kuondoa utozwaji wa bei kubwa kati ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Karatu (KARUWASA) na Mamlaka ya Utoaji wa Huduma ya Maji Vijijini (KAVIWASU)

Aweso ameyasema hayo wakati wa kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali wa maji ambapo awali inasemekana kulikuwa na mgawanyiko wa maslahi ikiwemo Kaviwasu kutoza uniti moja kwa sh,2000 hadi 3000 huku Karuwasa ikitoza sh,1,750 kwa bei za majumbani.

Alisema uwepo wa chombo kimoja kutawezesha maslahi ya wananchi kuzingatiwa ikiwemo utoaji wa huduma bora za utoaji maji pamoja na kuhakikisha miundombinu ya maji haiharibiki.

Ameongeza kuwa hakuna mtumishi yoyote atakayefukuzwa baada ya kuungana Karuwasa na Kaviwasa kwani watakapoungana lita zaidi ya milioni 6 zitakuwepo ndani ya mamlaka moja.

Hata hivyo aliagiza bei atakayotozwa mwananchi wa kawaida kwa hivi sasa iwe ni sh,1,300 kwa uniti 1 wakati Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji( Ewura) ikiendelea kuchakata bei halisi itakayotozwa kwa wananchi juu ya ulipaji wa ankara za maji katika mji wa Karatu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dadi Kolimba,alimshukuru Waziri Aweso kwa kutoa maagizo hayo kwani wananchi watanufaika na bei moja badala ya awali kuwa na mkanganyiko wa bei kati ya Karuwasa na Kaviwasu

Alisema baada ya Rais Samia kutangaza filamu ya Royal Tour watalii wamefurika wilayani Karatu na hivi sasa hoteli zaidi ya 60 zilizopo hapo zinahitaji maji hivyo aliomba wilaya hiyo kupewa zaidi vipaumbele vya maji ili kuwezesha kila mtu kunufaika na huduma za maji.

Naye,Ofisa Tawala Mkuu kutoka Wizara ya Maji,Jacob Kingazi akisoma mapendekezo ya kamati iliyoundwa na Waziri Aweso kwaajili ya kufanya tathimini ya hali ya upatikanaj wa huduma ya maji mji wa Karatu,alisema lazima kuwepo Kwa chombo kimoja kitakachosimamia utoaji wa huduma katika mji wa karatu

Pia walibaini bodi kuendelea kutekeleza baadhi ya majukumu ya kiutendaji ingawa ilifikia ukomo mwaka 2019 ikiwemo ukusanyaji wa mapato.Share To:

Post A Comment: