Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick (aliyesimama) akichangia jambo katika moja ya mikutano  ya kuhamasisha matumizi ya Lishe bora kwa watoto mkoani hapa.

Lishe bora kwa watoto wadogo ni suluhisho la udumavu kwa jamii kama afanyavyo mama huyu.

Lishe duni kwa watoto wadogo husababisha udumavu kama wanavyoonekana watoto hawa.


 

Na Abby Nkungu. Singida


SUALA la lishe duni kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano mkoani Singida huenda likabaki historia baada ya takwimu kuonesha kuwa tatizo sugu la udumavu kwa kundi hilo limepungua kwa asilimia 10 katika kipindi cha miaka minane iliyopita.

Kulingana na  taarifa  ya Utafiti wa Kitaifa wa Afya na  Demografia, kiwango  cha  udumavu kwa  watoto wa umri chini ya miaka mitano kimepungua kutoka asilimia 39 mwaka 2010 hadi  asilimia 29 mwaka 2018.

Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Victorina Ludovick anasema kuwa mafanikio hayo ni  matokeo chanya ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na idara ya afya na wadau wengine katika kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa lishe bora kwa mama na mtoto ili kupunguza tatizo la  udumavu katika jamii.

“Kama unavyojua hivi sasa Serikali inatekeleza Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) iliyoanza kutekelezwa Januari mwaka jana na inaendelea hadi mwaka 2026. Kwa hiyo, ni matumaini yangu hali itakuwa nzuri zaidi kwa watoto wetu” alieleza Dk Ludovick.

Alisema kuwa chini ya Programu hiyo, kila mdau amekuwa akitimiza vyema wajibu wake lengo likiwa ni kuharakisha upatikanaji wa matokeo chanya kwa kuboresha mfumo jumuishi wa sekta mbalimbali; ikiwemo afya bora, lishe, malezi yenye mwitikio, ulinzi na usalama na fursa za ujifunzaji wa awali kwa mtoto.

Dk Ludovick alisema kuwa pamoja na wadau wengine kutimiza vyema wajibu wao kupitia Programu Jumuishi, Serikali nayo kwa upande wake imeongeza bajeti  ya lishe kwa mtoto kwa kila halmashauri kutoka 1,000/- kwa mwaka wa fedha 2020/21 hadi 1,239/- kwa 2021/2022.

Hata hivyo, alisema kuwa licha ya juhudi hizo kusaidia kupunguza udumavu, bado kuna changamoto ya ukondefu wa watoto kwa asilimia 5.1 na uzito pungufu kwa asilimia 18.2 suala ambalo idara ya afya mkoa inaendelea kulifanyia utafiti juu ya sababu zake ili iweze kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti changamoto hiyo.

Daktari bingwa Mshauri wa magonjwa ya wanawake na watoto katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida, Dk Suleiman Muttani anasema pamoja na tafiti kuendelea kufanyika, mara nyingi suala la udumavu, ukondefu na uzito pungufu ni matokeo ya lishe duni na huleta homa za mara kwa mara kwa mtoto.

“Lishe duni ni chanzo kikubwa cha magonjwa na vifo kwa watoto wadogo na pia hudumaza ukuaji wa kimwili, kiakili na hupunguza uwezo wa mtoto kufanya vizuri shuleni na ufanisi wa kazi katika maisha ya utu uzima. Ndio maana msisitizo mkubwa huwekwa kwenye lishe bora kwa mtoto katika siku 1,000 za mwanzo; yaani tangu mimba kutungwa” alifafanua Dk Muttani.

Kwa upande wao, baadhi ya wazazi na walezi  wanasema kuwa cha muhimu ni kwa wataalamu wa afya na lishe kuendelea kutoa elimu kwa jamii; hususan Vijijini, juu ya umuhimu wa lishe bora hasa kwa akinamama wajawazito, wanaonyonyesha na  watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

“Fikiria katika karne hii eti bado kuna watu vijijini wanaamini mama mjamzito akila mayai atazaa mtoto asiyekuwa na nywele. Pia wanazuiwa kula maini kwa imani mbalimbali za kienyeji.  Elimu bado inahitajika sana katika suala la lishe", alisema Patrick Mdachi Ofisa Maendeleo ya jamii mstaafu na Mtafiti wa masuala ya mila na desturi katika jamii.

Rehema Daniel mkazi wa Ginnery na Tatu Athumani mkazi wa Kibaoni mjini Singida wanasema pamoja na elimu duni juu ya lishe bora, ugumu wa maisha bado ni changamoto nyingine kwani baadhi ya vyakula bora na muhimu vinahitaji rasilimali fedha ili kuvipata.

“Unapenda umnunulie mwanao maziwa ambayo lita moja ni kati ya 1,500/- na 2,000/-. Kwa mwezi lazima uwe na takriban 45,000/-. Hapo bado hujaweka  angalau yai moja la 500/- kwa siku na vyakula vingine kwani hata viazi lishe na matembele vinahitaji hela” alisema Rehema na kuungwa mkono na Tatu, huku wakiisihi Serikali kuangalia suala la mfumko wa bei.

Kwa mujibu wa Mganga mkuu wa mkoa Dk Ludovick, mbali na kutoa elimu ya lishe kwa jamii kupitia kamati za ngazi mbalimbali, mkoa wa Singida pia una vituo 99 vya kutolea huduma za matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto wenye ukondefu.  

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: