MAHAKAMA ya Wilaya ya Kinondoni imemuhukumu mtoto wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu , George Simbachawene, James George (24), kulipa faini ya jumla ya sh. 250,000 au kutumikia kifungo cha miaka miwili na nusu gerezani iwapo atashindwa kulipa faini hiyo baada ya ya kukiri kufanya makosa matatu ya Usalama barabarani.


Mshtakiwa George anayeishi eneo la Makumbusho mkoani Dar es Salaam pia amefungiwa leseni yake ya dereva kwa kipindi cha miezi sita.

Hukumu hiyo imesomwa leo Agosti 24,2022 na Hakimu Mkazi, Aaron Liyamuya.

Hati ya mashtaka imedai mshtakiwa anakabiliwa na kosa la kuendesha gari kwa kasi, kuendesha gari akiwa amelewa na tatu kuendesha gari pasipokuwa na bima.

Akisoma hukumu Hakimu Lyamuya amedai, ameridhika na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa Jamuhuri na pia mshtakiwa mwenyewe kukiri makosa yake na hivyo akatoa adhabu.

Hata hivyo, kabla ya kusoma adhabu hiyo, hakimu Lyamuya aliuliza upande wa Jamuhuri kama walikuwa na lolote la kusema ndipo, wakili wa serikali Daisy Makakala akaiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe funzo kwake na kwa wengine kwani alifanya makosa hayo akiwa na akili timamu huku akijua kuwa ni kinyume cha sheria.

Katika utetezi wake, mshtakiwa kupitia wakili wake, Alfred Mtawa ameiomba mahakama kumpunguzia mteja wake adhabu na pia isimfungie leseni yake kwani ajali hiyo haijasababisha majeruhi wala kifo cha mtu yoyote ni magari tu kuharibika aiomba mahakama hiyo kuzingatia adhabu kwa kuwa mtuhumiwa amekri makosa yake yote.

Naye mshtakiwa George alipopewa nafasi ya kujitetea yeye mwenyewe amekiri kutenda makosa hayo na kujutia makosa yake na ameomba huruma ya mahakama kwakua ni kosa la kwanza pia ana mke na mtoto mchanga ambao bado wanamtegemea

"Baada ya kusikiliza mashtaka na kuridhishwa na ushahidi na pia mtuhumiwa kukiri kuhusika na makosa haya, katika kosa la kwanza la kuendesha gari kasi mshtakiwa unatakiwa kulipa faini ya shilingi laki moja au kwenda gerezani mwaka mmoja na katika shtaka la pili adhabu yake ni faini ya Shilingi moja au kifungo cha mwaka mmoja na kosa la tatu utatakiwa kulipa faini ya shilingi elfu hamsini au kifungo cha miesi sita gerezani". Amesema hakimu Lyamuya

Pia mshtakiwa anafungiwa leseni yake ya udereva kwa muda wa miezi sita na kuamuru atafute njia mbadala ya yeye kufanya safar zake mpaka atakapojitathmini uendeshaji wake.

Mapema upande wa Jamuhuri uliwasilisha ushahidi wao na kudai kuwa, katika upelelezi uliofanyika mtuhumiwa aligundulika kunywa kiasi cha pombe cha 184.3mg/100ml baada ya kupimwa na kuendesha gari kutendo ambapo ni kinyume na sheria.

Vielelezo vyote vikiwepo katika ushahidi wa kesi hiyo ikiwemo leseni ya mtuhumiwa report ya tukio hilo ramani ya eneo hilo pamoja na taarifa za kipimo cha pombe

Katika shtaka la kwanza inadaiwa, Agosti 20 ,2022 mshtakiwa George akiwa maeneo ya barabara ya Haile Sallasie mtaa wa St Peter wilaya ya Kinondoni Dar Es Salaam aligonga gari lenye namba za usajili T 344 DKG aina ya Toyota IST.

Imedaiwa baada ya tukio hilo aliendesha gari kwa mwendo wa kasi na kwenda kugonga gari jingine lenye namba za usajili T370 DWY lililokuwa limesimama kwenye mataa na kusababisha madhara katika gari zote 


Share To:

Post A Comment: