Na Joachim Nyambo,Mbeya.


MKOA wa Mbeya umezindua rasmi Programu Jumuishi ya Kitaifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) tayari kwa kuanza kuutekeleza na kuleta ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla.


PJT-MMMAM ni programu inayetekelezwa nchini ikilenga kuleta uchechemuzi ndani ya jamii katika malezi ya msingi ya watoto kupitia vipengele vya Afya bora,lishe kamili,ulinzi na usalama,malezi yenye mwitikio na ujifunzaji na uchangamshaji wa awali wa mtoto katika umri wa tangu miaka sifuri hadi minane.


Akizindua programu hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Juma Homera,kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo,Said Madito aliihimiza jamii mkoani hapa kuwekeza zaidi kwenye malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya watoto ili kujenga msingi imara wa ukuaji timilifu wa watoto watakapofikia ukubwani.


Madito aliyataka makundi yote ndani ya jamii mkoani hapa kuhakikisha yanashiriki kwenye utekelezaji wa akisema kuwekeza katika umri huo wa mtoto ndiko kunawezesha taifa lolote kuwa na jamii iliyo kamilifu.


Alisema kutowekeza kikamilifu kwenye malezi ya awali ya mtoto ndiko kunapelekea baadhi ya jamii kuwa na watoto,vijana na watu wazima walio na changamoto nyingi na kuisababishia serikali kutumia nguvu nyingi kuwarekebisha.


Alizitaja changamoto zinazotokana na jamii kutowekeza kwenye umri mdogo wa watoto kuwa ni pamoja na uwepo wa watumiaji wa dawa za kulevya kama bangi,makahaba na matukio mengine ambayo hayana msaada kwenye jamii.


“Kwakuwa hii ni programu jumuishi ni shirikishi hatutarajii kundi lolote kwenye jamii litaachwa nyuma.. ndiyo maana mliopo humu kila mmoja ana taaluma tofauti tofauti.Kila aliyeyepo hapa hajaalikwa kwa bahati mbaya amealikwa kwa makusudi ili aweze kutimiza yale tunayokubaliana siku ya leo.” Alisisitiza Madito.


“Tukumbuke kuwa mwisho wa siku tutakuwa na utaratibu wa  kujipima sisi ini tulikifanya katika kutimiza majukumu yetu katika  malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.” Aliongeza.


Meneja mradi wa Shirika la Kihumbe lililopewa jukumu na Mkoa la uchechemuzi wa programu hiyo kupitia Mtandao wa malezi,makuzi na maendeleo ya  awali ya mtoto nchini(Tecden),Jeremiah Henry alisema mafanikio ya uzinduzi huo yametokana na ushirikishwaji wa pamoja baina ya sekretarieti ya mkoa na wadau wengine yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali.


Naye afisa miradi wa Shirika lisilo la kiserikali la CRS,Neema Haule pamoja na kupongeza uwepo wa viongozi katika ngazi ya mkoa walio na upeo mkubwa juu ya malezi na makuzi ya awali ya mtoto alisema kufanikiwa kwa program hiyo kutatokana na kila mmoja kwa nafasi yake kutambua kuwa analo jukumu la kuwa karibu na watoto.


Awali akitoa maelezo ya PJT-MMMAM,Afisa Maendeleo ya jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Salome Francis aliutaja mkoa wa Mbeya kuwa wa saba kuzindua progarmu hiyo kimkoa tangu ilipozinduliwa kitaifa Desemba mwaka jana.


Salome alihimiza mikoa iliyosalia kuhakikisha wanashirikisha wadau muhimu wote kwenye uzinduzi wa programu hiyo ili kuwezesha kuwepo kwa uelewa wa pamoja kwenye utekelezaji wake na kuwezesha matokeo chanya yanayotarajiwa.


Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: