Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana naShirika la Amref Health Africa Tanzania, na Wizara ya Afya ya Zanzibar, leo imeendesha kampeni ya ‘Uzazi ni Maisha Wogging Marathon’ katika Uwanja wa Sheikh Amani, Zanzibar, Tanzania.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Dr. Hussein Ali Mwinyi, alikuwa ndiye Mgeni Rasmi wa tukio hilo laMatembezi, Mbio Fupi na Ndefu (Wogging (Walk-Jog-Run)).

Kwakauli mbiu: Changia Vifaa Tiba kwa Uzazi Salama” matembezi, mbio fupi na ndefu (kwa kifupi‘wogging’) zilizopata umaarufu zilikazia kutoa elimu kuhusu upungufu uliopo katika sekta ya afya na kukusanya fedha ili kusaidia jitihada za serikali katika kuhakikisha kwamba vifaa tiba na dawa kwa uzazi salama vinapatikana katika vituo vya afya vilivyobainishwa hapa Zanzibar.

Kwa hiyo, tukio hilo lililolenga kuhamasisha taasisi za umma, makampuni na sekta binafsi, watu binafsi pamoja na wadau wengine kuchangia na kutoa msaada wa vifaa tiba na dawa kwa uzazi salama Visiwani.

Kampeni hiyo iliwawaleta pamoja zaidi ya washiriki 4,000 ambao ni pamojana maofisa wa ngazi za juu wa makampuni, wanadiplomasia, washirika wa maendeleo, maofisa wa serikali, vyombo vya habari na watu binafsi ambao waliotoa ahadi na kueleza utayari wao wa kusaidia kuchangia kampeni hii kupitia njia mbalimbali za utoaji msaada.

 Katika kipindi cha miaka mitatu, Kampeni ya Uzazi ni Maisha Wogging inalenga kukusanya zaidi ya Shilingi za Tanzania bilioni moja ikiwemo misaada ya vitu, fedha taslimu na ahadi za kutoa misaada ya vifaa tiba kwa uzazi salama. Kampeni itaendeshwa kwa miaka mitatu huku kukiwa na ushiriki wa wadau mbalimbali hadi hapo lengo litakapofikiwa.

Mgeni rasmi wa tukio hili, Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alipongeza juhudi za Amref kwa kubuni njia hiyo ya kipekee na kuwaasa wadau zaidi kushiriki ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya upatikanaji wa vifaa tiba na dawa kwa ajili ya uzazi salama hapa Zanzibar. Alisema michango hiyo mikubwa ni muhimu sana na msaada utakaotolewa utaelekezwa katika kuokoa maisha ya kina mama na watoto wachanga, na hivyo kupunguza vifo wakati wa uzazi, ambavyo vinaweza kuzuiwa hapa nchini.

“Idadi ya vifo vinavyotokana na matatizo ya uzazi vinavyowaathiri moja kwa moja akina mama na watoto wachanga bado iko juu hapa Zanzibar, ikiwa ni vifo vya akinamama 267 kati ya vizazi hai 100,000 kwa mwaka; na wastani wa vifo 28 vya watoto kati ya vizazi hai 1,000 kwa watoto wachanga (kutokana na takwimu za HMIS 2017).

 ”Huduma za mama na mtoto katika vituo vyetu vya afya zina changamoto nyingi ambazo zinachangia katika vifo hivi vitokanavyo na matatizo ya uzazi ikiwemo upungufu wa vifaa tiba, dawa nauhaba wa wahudumu wa afya”

 ”Nimetaarifiwa, Kupitia kampeni hii ya Uzazi ni Maisha, jumla ya vituo vya afya 28 vitapata vifaa tiba ambayo ni sawa na asilimia 40.5% ya vituo vyote vinavyotoa huduma ya mama na mtoto katika vijiji vilivyo hapa Zanzibar. Namhimiza kila mmoja ajitahidi kuwa sehemu ya mpango huu mwema na kuleta mafaniko kwa Serikali yetu ya Zanzibar,” alisema Mh. Mwinyi.

Vile vile, Dkt. Mwinyialiipongeza Benki ya NBC kwa kushirikiana na Amref Tanzania na kusaidia kampeni hiyo muhimu kwa kushirikiana na serikali ili kupunguza idadi vya vifo vya akina mama hapa Zanzibar.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi,akitoa hotuba yake alisisitiza kuwa wana dhamira kubwa ya kuboresha afya ya Mama na Mtoto “Benki ya NBC  pia tunaunga mkono ajenda ya taifa ya kuboresha  Afya ya mama na mtoto kupitia msaada wa Kliniki za Magari yaani (Mobile Clinic Vans) ambazo tumezitoa kwa serikali kupitia halmashauri za miji ya Unguja-Zanzibar na Dar es Salaam.

Kupitia Kliniki hizi, ambazo zilianzishwa mwaka 2020, tumefanikiwa kuwafikia jumla ya walengwa milioni tatu ambapo huduma zote hutolewa BURE.Gari jipya la Kliniki hizi tulilolitoa hapa Zanzibar mwaka 2021 limefanikisha kuwahudumia wakinamama na watoto zaidi ya milioni moja na nusu na hivyo kusaidia sana kupunguza vifo vya kinamama wakati wa kujifungua (Maternal Deaths).

Akizidi kufafanua , Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, alisema ushirika kati ya Amrefu na NBC ulikuwa na thamani kubwa na kiasi kilichochangwa na benki ni mwendelezo wa juhudi zabenki hiyo katika kutimiza sera yake ya kurudisha kiasi cha faida kwa jamii (CSR) kunakosukumwa na utayari wa kushirikiana na jamii ambamo benki inatoa huduma ili kuimarisha sekta ya afya, hasa akitaja afya ya uzazi kama moja ya nguzo kuu za sera hiyo ya NBC. Benki ya NBC imeguswa na changamoto mbalimbali zinazokabili huduma za afya na elimu hapa Zanzibar, alisema, akisisitiza kwamba benki inashirikiana na serikali mbili ili kutatua changamoto zinazozikabili sekta hizo mbili.

Kwa upande wake,Dkt. Florence Temu, Mkurugenzi Mkazi waAmref Health Africa Tanzania alisema: “Sisi, Amref, kwa kushirikiana na Benki ya NBC nawizara ya afya Zanzibar tumeandaa kampeni hii ya‘Uzazi ni Maisha Wogging’, kwa mkazo wa kusaidia upatikanaji wa vifaa tiba muhimu kwa ajili ya uzazi salama hapa Zanzibar, jambo lililo la msingi katika kuokoa maisha ya mama na mtoto, hasa katika mikoa mitano ya Zanzibar ambayo ina  matukio mengi ya vifo vitokanavyo na uzazi.

 Mikoa hiyo ni Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kusini Pemba na Kaskazini Pemba. Takribani vituo 28 vya afya vitanufaika na uchangishaji huu. Kupitia kampeni hii, Amref inatarajia kuchangisha fedha kwa miaka mitatu ijayo mfululizo (2022 – 2024) katika kusaidia kuimarisha eneo hili la afya ya mama na mtoto. Katika mwaka huu wa 2022, malengo ni kukusanya zaidi ya Shilingi za Kitanzaniabilioni 1 (USD 431,031) ili kuhakikisha kwamba mikoa mitano iliyobainishwa inapatiwa vifaa tiba na dawa.”Alitoa wito kwa umma wa Watanzania kuendelea kuunga mkono mpango huu mwema na kuwa sehemu ya kuokoa kizazi kijacho, viongozi watarajiwa na amana ya taifa kwa kuchangia kupitia namba ya Vodacom ya 5529421 au wavuti maalumu wa mchango wa hisani wa wogging ambao ni https://wogging.amref.org/

Share To:

Adery Masta

Post A Comment: