Na,Jusline Marco;Arusha

Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF imetekeleza mradi wa ujenzi wa kivuko katika kitongoji cha Moivo kata ya Moivo halmashauri ya Arusha, changamoto ambayo ilihatarisha maisha ya watu na mali za wakazi wa eneo hilo.

Akizindua kivuko hicho Mkurugenzi Mtendaji  Halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi amewataka wananchi wa Kata ya Moivo, kukitunza kivuko hicho ili kiweze kudumu na kuwaletea mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kwa kuwa tayari serikali imetimiza jukumu lake la kuwawekea miundombinu hiyo.

Kwa upande wao wananchi wa Kata ya Moivo licha ya kuishukuru TASAF kwa kuwajengea kivuko wameeleza madhara yaliyowapata kabla ya kuwa na kivuko,kuwa ni watu kuporwa mali zao na vibaka, wanawake kubakwa huku wengine wakinusurika kuuawa pamoja na watoto kushindwa kwenda shule hasa wakati wa mvua kwa kushindwa kupita hapo.

Eliamani Shange ambaye ni mnufaika wa TASAF ameweka wazi  kuwa uwepo kwa kivuko hicho sasa kumeondoa kero zote na kubwa zaidi sasa watoto watakwenda shule kwa amani huku kivuko hicho kikitarajiwa kukuza uchumi wa eneo hilo kwa kuwa wafanyabiashara watasafirisha bidhaa zao kwa urahisi tofauti na hapo mwanzo.


"Kivuko hiki kimetusaidia sana kina mama na watoto lakini pia  kimewarahisishia wajasiriamali kusafirisha bidhaa zao kama unavyoona magari sasa yanapita hapa yamebeba bidhaa mbalimbali, zamani watu tulibeba kichwani tunaishukuru sana TASAF ni mkombozi wa jamii na mali zao usafiri ni wa uhakika usiku na mchana"Ameeleza Mwajabu Hassan

Naye Diwani wa kata ya Moivo Mhe. Selina Mollel ameipongeza serikali kupitia TASAF kwa kuwaondolea wananchi wake kero ya muda mrefu sambamba na kuwapongeza walengwa wa TASAF kwa kujenga kivuko hicho kwa mikono yao kupitia mpango wa ajira za muda unaowawezesha walengwa kufanya kazi katika miradi hiyo

"Niwapongeze walengwa wa TASAF mmefanya kazi kubwa na nzuri mmesimama imara ya kuhakikisha kivuko kimepatikana kama lilivyokuwa hitaji lenu la muda mrefu,mmefanya kazi kwa moyo bila kukata tamaa hadi ujenzi umekamilika serikali yetu inahitaji wananchi wazalendo kama ninyi"  Amesisitiza Mhe. Selina.Awali mradi wa Kivuko cha Moivo umetekelezwa na TASAF kupitia programu za ujenzi wa miundombinu na Ajira za muda kwa gharama ya shilingi milioni 68 huku asilimia 50 ya fedha hizo zikitumika kununua vifaa na asilimia 50 ikitumika kulipa ujira kwa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini kwa lengo la kuwaongezea kipato.

Share To:

JUSLINE

Post A Comment: