Ikiwa ni siku chache baada ya filamu ya Tanzania "The Royal Tour” kuzinduliwa, tathmini inaonesha kuwa kuna ongezeko kubwa la watalii wanaokuja nchini Tanzania kwa ajili ya shughuli za utalii.


Akizungumza na waandishi habari leo jijini Dar es salaam mara baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Katibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka amesema ongezeko hilo ni mafanikio kwa sekta ya utalii hivyo Watanzania waendelee kujitokeza kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya utalii wa ndani.

Katika maonesho hayo Prof. Sedoyeka amefurahishwa na maandalizi mazuri na maendeleo yaliyopatikana katika Sekta ya Maliasili na Utalii na kutoa wito kwa watanzania wote watembelee maonesho hayo hususani banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kujifunza na kupata taarifa mbalimbali za sekta hiyo.

"Leo nimepita katika mabanda yetu ya maonesho ya sabasaba na kuona hali ilivyo na mimi mwenyewe kutalii, nimefurahishwa sana na kiwango cha maandalizi na bidhaa mbalimbali ambazo zinaoneshwa humu ndani zikiwemo za wajasiriamali mbalimbali"

Prof. Sedoyeka ametumia fursa ya ujio wake kwenye maonesho hayo kuwaalika wananchi waendelee kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na wizara na taasisi zake pamoja na wadau mbalimbali katika masuala ya uhifadhi wa Maliasili, Malikale na Uendelezaji Utalii.

"Watu wote watakaofika katika banda letu la maliasili hapa sabasaba watapata huduma za chakula kutoka chuo cha Taifa cha Utalii lakini kikubwa watapata kuona wanyamapori mbalimbali wakiwemo chui, fisi, mamba na aina mbalimbali za wanyamapori wanaotambaa kama kobe na nyoka wakubwa"Share To:

Post A Comment: