Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 40,000 kwa wakulima na wananchi wanaoishi kando kando ya hifadhi za Taifa huku ukilenga kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za Taifa, vivutio vya kiutamaduni na mambo kale nchini.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Mhe Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) Mkoani Iringa alipokua akizindua mfumo wa kushughilikia malalamiko yatokanayo na shughuli za mradi wa REGROW unaotekelezwa na  Wizara ya Maliasili na Utalii.


Aidha Mhe. Balozi Chana amesema uwekezaji wa mradi huo unaenda sambamba na juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suhulu Hassan za kuutangaza utalii kupitia “Royal Tour” kwa kuandaa mazingira wezeshi ya uwekezaji katika sekta ya utalii na sekta nyingine nchini.


“Utekelezaji wa mfumo huu unategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wetu kama wadau wakuu katika utekelezaji wa mradi wa REGROW, hivyo ninaomba tuutangaze mfumo huu na kuutumia kuwasilisha maoni na malalamiko yatakayotokana na utekelezaji wa mradi wa REGROW” Alisisitiza Mhe Balozi Chana.Share To:

Post A Comment: