Na,Richard Bagolele,Chato.


Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Martha Mkupasi leo amekabidhi nyumba 20 zenye thamani ya shilingi milioni 860 kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato.


Akikabidhi nyumba hizo kwa watumishi hao, Mkuu Wilaya amewataka watumishi hao kuzitunza vizuri nyumba hizo ili ziweze kudumu ambapo ameutaka uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha wanaweka uzio katika nyumba hizo kwa ajili ya usalama wa watumishi hao.


"Nyumba hizi ni nzuri, tunatakiwa kuzitunza vizuri nyumba hizi pamoja na miundombinu yake ili ziweze kudumu" amesisitiza Mkuu wa Wilaya.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Dokta Brian Mawalla  amesema kukamilika kwa nyumba hizo 20 ni mwanzo wa maandalizi ya ujenzi wa nyumba zingine 20 ambapo amesema tayari wameomba fedha. Ameongeza kusema watumishi waliopewa kipaumbele kwenye nyumba ni wale wanaotoa huduma za dharula hospitalini hapo.


Dokta Mawalla ameishukuru serikali kupitia wizara ya Afya kwa kuendelea kuipatia fedha nyingi hospitali hiyo ambapo amesema kukamilika kwa nyumba hizo kutasaidia kutatua changamoto kubwa ikiyokuwepo ya utoaji wa huduma za dharula ambapo hapo awali ilikuwa ni vigumu kuwapata watumishi kwa haraka.


Nao watumishi waliokabidhiwa nyumba hizo wameishukuru serikali kwa uamuzi wa kujenga nyumba hizo kwani zitasaidia kutatua changamoto nyingi zikiwezo za usafiri, umbali na hospitali na kodi za nyumba.


"kukamilika kwa nyumba hizi kutasaidia sana kwetu sisi kuhudumia wagonjwa wa dharula kwani hivi sasa tumesogea karibu na hospitali itaturahisishia kufika hospitali kwa wakati" amesema Dokta Muyenjwa.


Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato ilianza kutoa huduma mnamo mwezi Julai 2021 ambapo hadi sasa ina jumla ya watumishi 144.

Share To:

Post A Comment: