Mbunge wa Jimbo la Songwe, Philip Mulugo.


 

Na Thobias Mwanakatwe

 

MBUNGE wa Jimbo la Songwe, Philip Mulugo, ameahidi kutoa Sh.milioni tatu kwa ajili ya kununulia injini ya boti ili kuwasaidia wavuvi wa Kijiji cha Iyovyo wanaovua samaki Ziwa Rukwa.

Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho katika mwendelezo wa ziara yake ya kuhamasisha maendeleo jimboni mwake,  alisema atatoa fedha hizo mwezi Oktoba mwaka huu na kuwataka wavuvi nao waanze kuchonga mtubwi.

Mulugo aliwataka wavuvi ili waweze kupata mikopo zaidi inayotolewa na halmashauri pamoja na Benki ya NMB wajiunge katika vikundi ili waweze kutambulika na hivyo kuwa rahisi kukopesheka.

"Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameruhusu mapato ya ndani ya halmashauri ya asilimia 10 yatumike kukopesha vikundi vya akiba mama na vijana, na pia benki ya NMB inakopesha vikundi na dhamana inakuwa ni kazi mnayoifanya," alisema Mulugo..

Mulugo ambaye amekuwa akitimiza ahadi anazotoa kwa wakati, alisema wavuvi hao watakapojiunga katika vikundi atasimamia kuhakikisha wanapata mkopo wa fedha ambazo zitawawezesha kununulia boti ya kuvulia samaki.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: