Mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini Timotheo Mnzava akizungumza na wananchi wa kijiji cha Tabora.


MBUNGE wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mnzava, amewataka wananchi wa jimbo hilo kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, kwa vile amepanga kuzitekeleza ahadi zote zilizoahidiwa katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020/2025.

Akizungumza katika mikutano ya hadhara ya vijiji vilivyopo katika kata ya Mswaha, mbunge huyo alisema kwamba ahadi zote zilizoahidiwa zitatekelezwa ili kuboresha maisha ya wananchi na kwamba juhudi anazofanya Rais hazina budi kuungwa mkono na wananchi.

Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Maurui, Tabora na Mswaha Darajani, Mnzava alisema katika kipindi cha mwaka mmoja na ushehee alichokaa Rais madarakani tayari ameonesha dhamira ya dhati ya kushughulikia matatizo na kero zinazowagusa wananchi na ambazo zimo kwenye ilani ya CCM na nyingine ametumia ubunifu wake kuzitekeleza.

Alisema mwaka 2020 wakati CCM ikiomba kura ilianisha kwenye ilani yake itaboresha elimu, afya, maji pamoja na miundombinu, lakini pia iliaahidi kumaliza changamoto zilikosa majawabu kwa muda mrefu.

Mnzava ambaye aliongozana na wakuu wa idara mbalimbali wa halmashauri ya Korogwe Vijijini, alisema Rais Samia anafanya kazi nzuri na anawapenda wananchi wa Korogwe na kwamba fedha katika miradi mbalimbali zinazoletwa ikiwemo ya elimu amekuwa akizitoa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na kuboresha mazingira ya shule.

Alisema wakati akiingia madarakani kulikuwa na kata 5 zilizopo katika jimbo hilo hazikuwa na shule za sekondari lakini kupitia Rais Samia wameweza kujenga shule mbili na nyingine zipo katika mipango ya kujengwa.

Alitaja shule zilizojengwa ni za kata ya Mgwashi na Makumba na kwamba katika kata zingine amehamasisha zijengwe ili watoto waweze kusoma katika maeneo karibu na vijiji vyao.

"Rais anafanya kazi na ana wapenda watu wa Korogwe, ombi langu kwenu tumuunge mkono Rais wetu na serikali yake na tuzidi kumuombea afanye makubwa zaidi ya haya kwa ajili ya Watanzania," alisema mbunge huyo.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mswaha Darajani, mbunge huyo alisema kwamba Rais Samia amekubali kutoa kiasi cha shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya ujenzi wa daraja ambalo litaunganisha kata ya Mswaha na kata ya Makuyuni kwa barabara inayotokea Kwasunga.

"Ndugu zangu ninapowaeleza kuhusu Rais wetu lazima mnielewe, ni mama aliyeandaliwa vizuri serikalini, ni mama aliyekuzwa na CCM kujali na kutazama maisha ya watu, tangu aingie madarakani mambo aliyoyafanya ni makubwa ambayo sisi kama Watanzania hatuna budi kumuunga mkono ili akamilishe kazi za kutuletea Maendeleo," alisema mbunge huyo.

Alisema fedha zilizoletwa kwa ajili ya daraja linalounganisha kata ya Mswaha na Makuyuni, mkandarasi aliyepewa kazi hiyo licha ya kujenga daraja hilo lakini pia barabara inayokwenda Mswaha itajengwa kwa moramu ili iweze kupitika vipindi vyote vya majira ya mvua na kiangazi.

Hata hivyo, mbunge huyo aliwataka wananchi wa kata Mswaha kuacha maneno ya kukatisha tamaa viongozi na badala yake wachangie maendeleo katika maeneo yao kwa faida ya vizazi vijavyo.

Mbunge huyo alisema maneno hayo baada ya diwani wa kata ya Mswaha Hassan Salim Mdigo, kulalamika kwamba kuna baadhi ya watu wanaleta uchonganishi baina ya viongozi na wananchi hali ambayo inasababisha wananchi wakose imani na viongozi wao.

Diwani wa Kata ya Kerenge, Shebila Idd Shebila alimpongeza Mbunge huyo kwa juhudi kubwa anayoifanya kupitia serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia ya kuwaletea wananchi Maendeleo hivyo akataka wananchi waendelee kuwaunga mkono.


Share To:

Post A Comment: