Baadhi ya Mataifa Nje ya Afrika yameomba kujiunga kama wanachama waangalizi katika Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Almasi Afrika  (ADPA) zikiwemo Taasisi zilizobobea kwenye masuala ya madini hayo.


Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko  wakati akifunga Mkutano wa Tatu (3) wa Dharula wa Baraza la Mawaziri wa jumuiya hiyo uliofanyika  jijini Arusha na kutanguliwa na mkutano wa wataalam kutoka mataifa wanachama.


Dkt. Biteko aliongeza kwamba suala hilo lilikuwa miongoni mwa ajenda tatu zilizojadiliwa katika mkutano huo na kwamba 

 jumuiya hiyo imepanga kuangalia sifa na vigezo  kwa nchi hizo na  wakati  utakapowadia italazimika kubadilisha Katiba  ya jumuiya hiyo ili kutoa fursa kwa nchi hizo kujiunga kwa lengo la kuendelea kujengeana uwezo na kubadilisha uzoefu na nchi zilizo nje ya Afrika katika masuala ya almasi.


Pia, alisema kuwa agenda nyingine  iliyojadiliwa katika kikao hicho ni kuhusu  Uteuzi wa watendaji wa kudumu katika Sekretatieti ya umoja huo ambapo Baraza liliamua  hadi kufikia katikati ya mwezi Septemba watendaji hao wawe wamepatikana.


Akizungumzia utaratibu wa ajira katika umoja huo, alisema mwananchi yoyote kutoka nchi wanachama anaruhusiwa kuomba  na kwa watu ambao wako nje ya mfumo wa Serikali watatakiwa  kupata idhini ya Serikali.


Aliongeza kwamba, agenda nyingine iliyojadiliwa ni kupitiwa upya na kuidhinishwa kwa Katiba ya jumuiya ambayo itawezesha kutekelezwa kikamilifu kwa matakwa ya jumuiya hiyo.

Katika hatua nyingine, washiriki wa mkutano huo walipata fursa ya kutembelea katika hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro kujionea vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo.

Katika Mkutano wa Tatu wa Dharura wa Baraza la Mawaziri, Tanzania ilikuwa nchi mwenyeji na Mwenyekiti wa sasa wa umoja huo.

Share To:

Post A Comment: