Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida, Florence Mwakasege, akizungumza na waandishi wa habari kwa ajili ya kujitambulisha baada ya kuhamishiwa mkoa wa Singida akitokea mkoa wa Ruvuma na kutoa taarifa ya utendaji wa kazi wa shirika hilo mjini hapa leo Julai 6, 2022.
Afisa Uhusiano na Huduma  kwa  Wateja wa Tanesco Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo,akizungumza kwenye mkutano huo na waandishi wa habari.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Mkutano ukiendelea. Kulia ni Afisa Utumishi wa TANESCO, Deogratias Jackson.
Wafanyakazi wa TANESCO Singida wakiwajibika.
Wafanyakazi wa TANESCO wa Kitengo cha Dharura wakiwajibika. Kushoto ni Solomoni Kangopa na Kokugonza Peter.
Mwonekano wa jengo la Ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singiga.


Na Dotto Mwaibale, Singida


HUDUMA mpya ya kuomba umeme iitwayo NIKONEKT imeleta mafanikio makubwa kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Singida ambapo kwa kipindi cha siku 37 shirika limepokea maombi 2,500 ya watu wanaohitaji kuunganishiwa huduma ya umeme.

Hayo yameelezwa leo na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Singida, Florence Mwakasege, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa ajili ya kujitambulisha baada ya kuhamishiwa mkoa wa Singida akitokea mkoa wa Ruvuma na kutoa taarifa ya utendaji wa kazi wa shirika hilo.

Alisema huduma hiyo tangu imeanza Mei 30, mwaka huu katika Mkoa wa Singida, hadi kufikia juzi Julai 6, takribani siku 37 Tanesco imepokea maombi 2,500 ya wahitaji wa umeme na kwamba kwa siku wanaolipia ni takribani wateja 70.

Alisema kati ya wateja waliomba huduma kupitia mfumo wa NIKONEKT waliolipia ni 930 na wateja 606 wameshaunganishiwa huduma ya umeme na kazi inaendelea kufanyika.

Mwakasege alisema Mkoa wa Singida umejaliwa kuwa na kiwango kikubwa cha umeme lakini watumiaji bado ni wachache ambapo kiwango kinachotumika ni Megawati 15 wakati kiwango kilichopo cha umeme ni megawati 100.

"Nitowe wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika Mkoa wa Singida tuna umeme wa kutosha kuweza kuwafikia na kuwahudumia kadri watakavyohitaji,umeme upo mwingi sana msitumie umeme kwa kuwasha taa tu tumieni hata kwenye saluni na viwanda vidogo," alisema.

Aidha, Meneja huyo wa Tanesco alitoa onyo watu wanaosafisha mashamba wakati wa misimu ya kilimo kuwa waangalifu wasiunguze miundombinu ya umeme.

"Mwananchi ambaye tutamkamata amechoma moto eneo lake akaunguza miuondombinu atachukuliwa hatua za kisheria na vyombo vya usalama vina taarifa na vimejipanga," alisema.

Mwakasege aliwaomba wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya Tanesco kwani miundombinu siyo mali ya Tanesco ni ya Serikali ambayo inajumuisha wananchi.

Katika hatua nyingine Mwakasege ametoa onyo kwa wakandarasi wanao weka mfumo wa umeme (wiring) katika ujenzi wa nyumba za kuishi kuwa wafuate taratibu ambazo zinaekeleza kwenye leseni zao kwani maeneo mengine Tanesco wanafika na kukutata nyumba hazijawekwa mfumo huo huku mkandarasi akiwa amepitisha fomu kuwa nyumba husika imekwisha kamilisha kazi hiyo na kusababisha shirika kutumia gharama kubwa ya kufika eneo husika.

“Nina wakumbusha utendaji kazi wa wakandarasi mimi nitachukua hatua na halitavumilika kwa mkandarasi yeyote atakayeenda kinyumme na kazi na miongozo inayotakiwa tutachukua hatua ikiwa ni pamoja na kumfutia kufanya kazi na Tanesco na pia tutawajulisha na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) “ alisisitiza Mwakasege.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: