Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir Ali Maulid akizungumza na wajumbe wa Baraza hilo pamoja na wageni waalikwa wakati akizunduza semina ya siku moja kwawawakilishi hao iliyoendeshwa na Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) kwa kushirikiana na wadau wengine visiwani humo ikilenga kuwajenga uelewa wajumbe hao kuelekea uanzishwaji wa huduma mpya ya Bima ya Kiislamu ‘Takaful’. Wanaomsikiliza ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango –Zanzibar Mhe. Dkt Saada Mkuya (wa tatu kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar(ZIC) Bw Arafat Haji (Kushoto) na wadau wengine.




Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango –Zanzibar Mhe. Dkt Saada Mkuya akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na wageni waalikwa wakati wa semina ya siku moja kwa wawakilishi hao iliyoendeshwa na Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) kwa kushirikiana na wadau wengine visiwani humo ikilenga kuwajenga uelewa wajumbe hao kuelekea uanzishwaji wa huduma mpya ya Bima ya Kiislamu ‘Takaful’.


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar(ZIC) Bw Arafat Haji akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na wageni waalikwa wakati wa semina ya siku moja kwa wawakilishi hao iliyoendeshwa na shirika hilo kwa kushirikiana na wadau wengine visiwani humo ikilenga kuwajenga uelewa wajumbe hao kuelekea uanzishwaji wa huduma mpya ya Bima ya Kiislamu ‘Takaful’.


Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa na wadau wa Bima ya Kiislamu ‘Takaful’.

..........................................

Na Mwandishi wetu-Zanzibar

Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) kwa kushirikiana na wadau wengine visiwani humo limeendesha mafunzo ya kujenga uwezo kwa wajumbe wa Baraza la wawakilishi Zanzibar ikiwa ni moja ya hatua muhimu kuelekea utoaji wa huduma yake mpya ya Bima ya Kiislamu ‘Takaful’.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika eneo Chukwani nje kidogo ya jiji la zanzibar, yalitanguliwa na mafunzo ya siku moja kwa mawakala wa bima visiwani humo yaliyofanyika visiwani Pemba huku lengo likiwa ni kuwaandaa wadau muhimu kuelekea kuanza matumizi ya bima ya kiislaam nchini.

Akizindua mafunzo hayo Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir Ali Maulid alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuleta mabadiliko katika kukuza huduma za bima ya kiislamu nchini huku akibainisha kuwa tayari nchi nyingi duniani zimeshafanya mabadiliko ya sheria za kifedha na kodi hivyo hatua hiyo itaweza kuweka mazingira bora ya kukuza na kustawisha huduma hizo.

“Ni imani yangu kuwa mfumo huu utaenda kuleta mabadiliko makubwa katika sekta za kibima hivyo ni wajibu wa serikali kuweka mikakati imara ili kuhakikisha wanachi walio wengi wananufaika” alisema,

Zaidi Mh Zubeir aliwahamasisha wajumbe wa baraza hilo kuhakikisha wanayatumia vema mafunzo hayo ili kujijengea uelewa wakutosha ili pia na wao waweze kupeleka uelewa huo kwa wananchi.

“Naamini pia kupitia uelewa huo mtaweza kuuliza maswali ya kina pamoja na kutoa maoni yenu muhimu kuhusu huduma hii ili wataalamu waweze kuyazingatia na kuyatekeleza kwa maslahi ya wananchi wetu hapa Zanzibar na taifa kwa ujumla,’’ alisisitiza.

Aidha Mh Zubeir alitoa wito kwa Mamlaka mbalimbali zinazohusika katika kufanikisha mpango huo zikiwemo taasisi za kifedha na mamlaka husika kuhakikisha zinafanya juhudi za makusudi ili kuruhusu utoaji wa huduma hiyo haraka iwezekanavyo lakini pia kwa ufanisi unaotakiwa ili iwe na tija zaidi hususani kwa wananchi wa kipato cha chini.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar(ZIC) Bw Arafat Haji alisema kupitia mkakati wa uendeshaji wa mafunzo hayo Shirika hilo linaamini kuwa taarifa muhimu kuhusu huduma hiyo mpya zitawafikia walengwa wote kote nchini ili waweze kuichangamkia pindi itakapowafikia.

“Ni matumaini yetu kuwa ujio wa huduma hii ya Bima ya Kiislamu yaani ‘Takaful’ itakuwa ni suluhisho sahihi la kuwavutia wananchi wengi zaidi visiwani Zanzibar na maeneo mengine ya nchi ambao kimsingi wanahitaji huduma ya Bima ila wanashindwa kutokana na imani za kidini.’’ Alisema

Alibainisha kuwa wananchi wengi wa visiwa vya zanzibar wamekua wakisuasua kuingia katika mifumo ya bima kwa kujiepusha na riba ambazo zimekuwa zikienda kinyume na silaka na dini zao.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya serikali na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango –Zanzibar Mhe. Dkt Saada Mkuya Salum pamoja na kuwapongeza wadau hao wakiwemo ZIC alisema semina hiyo imeendeshwa kwa kundi muhimu kwa kuwa wajumbe hao wanawakilisha maelfu wa wananchi hatua itakayorahisisha usambazaji wa elimu hiyo.

“Baada ya mafunzo haya sisi kama viongozi wa serikali pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi tunabaki na jukumu kubwa la kuhakikisha elimu hii haibaki miongoni mwetu bali inawafikia wananchi tunaowawakilisha huko majimboni na hicho ndio kitu kinachofuata baada ya hapa. Huduma hii ni muhimu sana kwa wananchi wetu na tutahakikisha inawafikia kama ilivyokusudiwa,’’alisisitiza.

Mbali na ZIC wadau wengine waliohusika katika utoaji wa mafunzo hayo kuhusu Bima hiyo inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni ni pamoja na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Kituo cha Usimamizi wa Masuala ya Huduma za Kifedha za Kiislamu na Ushauri Tanzania (CIFCA) na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu(IsDB).
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: