Mkurugenzi wa huduma za mifugo kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga wakati akizindua,kulia kwake ni Mkurugenzi wa shahada za juu, utafiti na ushauri wa kitaalamu kutoka SUA Prof. Esron Karimuribo na kushoto kwake ni Mtafiti kiongozi wa Programu hiyo Prof. Robinson Mdegela. Mtafiti Kiongozi wa Progamu hiyo ya Utafiti Prof. Robinson Mdegela kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine amesema program akieleza malengo ya Progamu hiyo na umuhimu wake. Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada za Juu, Utafiti na ushauri wa kitaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Hesron Karimuribo akitoa Salamu za SUA kwa washiriki wa Mkutano huo.

Picha ya Pamoja na wadau na washiriki wote kwenye mnyororo mzima wa thamani wa ufugaji wa kuku wa kisasa wa Nyama na Mayai,Wizara ya afya,Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Watafiti wa Miradi yote miwili na Taasisi za utafiti na uzalishaji wa Chanjo.

Wadau hao wakifuatilia maneno na uzinduzi wa Programu hiyo.

*****************************

Na: Calvin Gwabara na Amina Hezron – Morogoro.

Wizara ya Mifugo na uvuvi imewapongeza watafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kuanzisha program inayolenga kuhakikisha usalama wa kuku wa Kisasa wa nyama na Mayai ili kulinda afya za watumiaji na mazingira nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa huduma za mifugo kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga wakati akizindua Program hiyo ya kudhibiti ongezeko la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa kwa njia ya kinga na kanuni bora za ufugaji na hatimae kudhibiti uchafuzi wa mazingira kutokana na samadi yenye mabaki ya dawa (VABIEN – ARM PROGRAMME).

Prof. Nonga amesema kuwa mradi huu utasaidia kuja na majibu mengi ambayo yamekuwa yakiwasumbua wafugaji wa kuku wa kisasa pamoja na walaji kuhusu usalama wa kuku hao kwa walaji lakini pia mbinu bora za ufugaji ambazo zitasaidia wafugaji kufuga kisasa na kupunguza matumizi makubwa ya dawa yasiyo ya lazima ambayo ni hatari kwa afya.

“Sisi wadau wa mradi huu ambao tunashiriki kwenye utekelezaji wake hasa wafugaji wa kuku hawa nchini tukasaidie kutoa yale yanayotarajiwa yaweze kupatikana ili tukapate muafaka, mkumbuke tunafanya kazi ya kitume maana ukiendelea kuwalisha wat una Antibayotiki kupitia mazao ya Mayai na Nyama alafu hao watu vimelea vikapata usugu dhidi ya dawa wakapelekwa hospitali na dawa zisiwasaidie alafu wakafa Mungu pia hapendi” alieleza Prof. Nonga.

Amesema taarifa za kina zinaonesha ongeeko la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa ni mkubwa hasa kutoakana na dawa za antibayotiki zinazotumia kila siku hivyo ni wakati sasa wa kusema imetosha na tusaidienae katika kutokomeza tatizo hili nchini.

“Tunatamani kujua kuku anaposhindwa kufanya vizuri na kudumaa bandani ni sababu ya chanjo peke yake? Au ni kwa sabau amekosa usafi? Maana kama chakula anakula na tunaambiwa kuku anayekula vizuri anakuwa na kinga yenye nguvu na kwa sababu tunaongelea swala la kinga na kinga inapatikana kwenye lishe bora kwahiyo tutasikia mengi sana kutoka huko” alisema Prof. Nonga.

Amesema ni matanio yao kuwa wafugaji watumie sana Chanjo maana kingani bora kuliko tiba lakini bado wanajiuliza hizo chanjo wanazowaaambia wazitumie zina ubora kiasi gani maana kumekuwa na matukio mfugaji anachanja kuku wake lakini bado kuku wanaugua na kufa banda zima na kupelekea kupoteza Imani na chanjo kwahiyo haieleweki kama ni mfugaji kakosea masharti au wasambazaji wa chanjo waliifadhi vibaya.

Kufuatia matokeo ya utafiti huu ndiyo yatakayotoa muelekea wa nini kifanyike katika maswala mazima ya chanjo na matumizi ya madawa lakini pia aina za vyakula ili kuku hao waweze kuwa na afya njema na wasiugue na kupunguza matumizi ya dawa yasiyo na lazima.

“Siku mfugaji napokwenda kununua vifaranga vya kuku wa nyama au wa mayai kwa mzalishaji ananunua na begi zima la dawa linaambatana na vifaranga vyake na akifika vifaranga wanapewa chakula na ile dawa na anaamini bila dawa kifaranga hakiwezi kukua vitakufa,bila dawa kuku wa mayai hawezi kutaga mayai mazuri makubwa, na yule kuku wa nyama hawezi kufikia uzito wa kuchinjwa ndani ya wiki nne au tano kwahiyo tunaona hapo ipo shida na tutasikia kutoka kwenu kama wahusika na wafugaji alafu mradi utatusaidia” alibainisha Mkurugenzi huyo wa Huduma za mifugo Prof. Nonga.

Amesema mradi unaweza usimalize mambo yote kwenye ufugaji wa kuku lakini baada ya miaka hiyo mitatu ya utekelezaji wake utakuwa umechangia kupunguza kumaliza kabisa changamoto fulani katika ufugaji wa kuku nchini.

Ameongeza kuwa kuna watengenzaji wengi vya vyakula na wazalishaji wengi pia wa vifaranga na kila mmoja anajisifia kuwa bora kumzidi mwenzie kwenye vifaranga na kwenye chakula lakini hatujawahi kufanya utafiti kujua ukweli wa hayo wanayojinasibu nayo.

“Tanzanaia tuna zaidi ya kampuni 26 za uzalishaji wa vifaranga na wengine ukinunua vifaranga kwake anakupa na nyongeza ya hadi robo ya vile ulivyochukua maana anajua kiwango cha vifo ni vikubwa kwa vifaranga wake hivyo hao wa nyongeza watakusaidia kurudiashia wale asilimia 40 watakaokufa lakini kwanini kifaranga afe? na kwa nini makampuni mengine vifaranga hawafi? aliuliza Prof. Nonga.

Amesema lengo ni kupunguza changamoto za ufugaji ili wafugaji wapate faida kwa mradi kutoa majibu ya changamoto hizo lakini pia ni kuhakikisha mlaji wa kuku hao na mayai hali kemikali zisizokuwa za lazima maana kuna mtu anazalisha mayai 500 au 1000 kwa siku lakini kuku hao wanakula antibayotiki na sharia ya tiba ya mifugo inasema utupe mayai hayo ndani ya siku saba kwa sababu yana masalia ya dawa lakini ni wafugaji wangapi wanatupa mayai hayo na ukifuatilia unakuta hakuna hata mmoja wakati mayai yanaliwa na nyama za kuku zinaliwa kila siku.

Akizungumzia mbolea itokanayo na kuku hao amesema kuwa nayo imekuwa kero na vurugu kubwa kwa jamii zinazozunguka wafugaji kwani zinatoa harufu na mbolea imekuwa nyingi na hawana mahali pa kuipeleka maana kuku wanakula sana chakula na kujisidia kwa kiasi kikubwa.

Amepongeza Mradi huu kwa kuona umuhimu wa kushughulikia swala la uchakati wa samadi hiyo ya kuku ili iweze kuwa salama kwa watu na mazingira kwa kutumia mbinu mbalimbali za kisayansi ambazo mradi utazitumia.

“Wakulima wa bustani hasa mboga mboga nao wanachukua mbolea hiyo ambayo nayo unakuta imejaa madawa na kwenda kuweka kwenye bustani zao za mboga mbona na mboga zinafyonza dawa hizo na kisha zinakwenda kuingia kwenye miili ya watumiaji na kusababisha watumiaji pia kupata usugu wa vimelea dhidi ya dawa na hivyo kuongeza tatizo kwa kula mboga na matunda yasiyo salama yenye antibiotiki na unakuta na nyanya zimepuliziwa madawa unachanganya kutengenza kachumbari watu wanakula na inapelekea watu kupata magonjwa hatari kama vile kansa na mengineyo” alifafanua.

Kwa upande wake Kiongozi wa Progamu hiyo ya utafiti Prof. Robinson Mdegela kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine amesema program hiyo ni ya miaka mitatu na ndani yake ina miradi miwili ambayo ni Mradi wa Kinga na matumizi mbalimbal ya kibiolojia ili kupunguza magonjwa kwa kuku na kuzuia matumizi makubwa ya dawa kwa kuku na Mradi wa pili unahusu mbinu za uchakataji wa samadi ya Kuku ili kulinda afya na mazingira.

Prof. Mdegela amesema Miradi yote miwili iliyo ndani ya Programu hiyo inalenga kutafuta majibu ya changamoto za ufugaji wa kuku wa kisasa wa nyama na mayai ili kupunguza athari zinazotokana na matumizi makubwa ya madawa kwa kuku ili kulinda afya ya watu na Mazingira lakini pia kutokomeza tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa.

“Takwimu zinaonesha mwaka 2050 kama jitihada za makusudi hazitafanyika kutakuwa na vifo vingi duniani ambavyo vinakadiriwa kufikia zaidi ya milioni 10 kwa mwaka kutokana na usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa na kupelekea kupoteza watu, Kuongeza umasikini,kupunguza uzalishaji na kuongezeka kwa gharama za kutibu watu Hospitalini”alifafanua Prof. Mdegela.

Aliongeza “Kwa sasa tatizo kubwa lipo nchi za Asia na Afrika lakini ni tatizo la kidunia na kwa sasa watu 700,000 wanakufa kutokana na tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, wakati mwaka 2050 watakuwa milioni 10 na litakuwa ndio tatizo kubwa kuliko tatizo linguine likifuatiwa na kansa”.

Amesema takwimu zinaonesha ongezeko kubwa la ulaji wa Nyama na Mayai toka mwaka 2010 hasa ikizingatiwa kubwa idadi kubwa ya watu ni vijana ambao wanapenda vyakula hivyo na hivyo kupelekea kuwa na ongezeko la uzalishaji wake kutokana na kipato cha watu kuongezeka hivyo lazima vyakula hivi view salama la sivyo jamii na nguvukazi ya taifa itaangamia.

Profesa Mdegela amesema mujibu wa taarifa za matumizi ya dawa za antibayotiki nchini kati ya mwaka 2002 na 2007 zinaonesha kuwa nchi ilitumia kilo milioni 12,147,491 na katika kilo hizo dawa ya Tetasacrine ya mifugo pekee ilikuwa milioni 8 na hayo ni makadirio ya chini maana zile zilizopita kwa njia ya panya hazikuhesabiwa.

“Tatizo haliishii tu kwenye mifugo bali tafiti zinaonesha kuwa asilimia zaidi ya 80 ya mbolea ya samadi ya kuku wa Nyama na Mayai inamabaki ya dawa na mbolea hiyo hutimika kwenye bustani za mboga na matunda ambazo nazo hufyonza dawa hizo zilizo kwenye samadi na kisha mtu akila mboga hiyo nae hupata madawa hayo lakini zipo teknolojia na kuchakata mbolea kuondoa mabaki hayo ya dawa na kuwa salama ambazo nchi za ulaya wanazitumia na wanataka kuona namna ya kuzijaribu mbinu hizo pia kupitia utafiti huo”aalifafanua Profesa Mdegela.

Prof. Mdegela amesema kuwa kwakuwa kuna muingiliano wa kiikolojia kati ya binadamu,Wanyama na Mazingira njia pekee inayoweza kusaidia kuondoa tatizo la matumizi makubwa na holela ya dawa kwa kuku hao ni matumizi ya Chanjo, usafi sambamba na kanuni bora za ufugaji wa kuku hao ili wasiugue.

Amesema jambo la msingi kabisa ni kupata majawabu yatakayoweza kusaidia wafugaji wetu wa kuku nchini kufuga vizuri lakini pia kupata majibu ya kitafiti ambayo yatawasaidia Watunga Sera na wafanya maamuzi na waende mbali zaidi kupata vitu ambavyo vitasaidia katika kusukuma sera ya viwanda hasa kupitia mbinu ambazo zitawezesha kuchakata samadi ya kuku na kuzalisha viwanda vya mbolea iliyo salama.

“Lazima kuzuia ongezeko la usugu wa vimelea dhidi ya dawa hasa unaotokana na matumizi makubwa na holela ya dawa za antibayotiki hususani kwenye kuku hawa wa mayai na nyama ambapo zinatumika sana maana tuna zaidi ya miaka 30 hakuna antibayotiki mpya iliyogunduliwa na hizi zilizopo wadudu wanazidi kutengeneza usugu kwahiyo wakimudu kutokufa kwa dawa kwa asilimia 100 watu wataumwa na dawa hazitawasaidia kabisa na wote tutakufa maana kutengeneza dawa hizo ni kazi” alieleza Kiongozi wa utafiti huo Prof. Mdegela.

Mwisho akifunga mkutano huo wa uzinduzi wa Programu hiyo, Daktari Mkuu wa Mifugo kwa upande wa Zanzibar Dkt. Talib Salehe Suleiman amesema mradi huo unemanufaa makubwa sana kwa watu wa Zanzibar kwakuwa sehemu kubwa ya Chakula kinatoka upande wa Tanzania Bara hivyo kikizalishwa chakula chenye shida na wao wataathirika.

“Zanzibari pia tunafuga kuku na changamoto zinazosemwa hapa na watafiti na wafugaji wa kuku pia zipo hivyo hivyo kwa upande wa Zanzubar na serikali imeendelea kupambana nazo lakini naamini kupitia mradi huu tutaweza kupata majawabu na hivyo kuwa mradi wa mfano katika matokeo yake” alieleza Dkt. Twalib.

Amesema ukika kwenye maduka ya pembejeo utakuta watu wananunu madawa lakini ukifika mitaani huoni mziwa yanayomwagwa,Mayai yanayotupwa wala kuku wanaotupwa na kwamba inaonesha dawa wanapewa mifugo alafu zinawarudia watu waliozitoa.

Progamu hiyo ya (VABIEN – AMR) inafadhliwa na Taasisi ya Kimataifa inayoshughuikia majibu ya changamoto ya ongezeko la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (International Centre for Antimicrobial Resistant - ICARS) ya nchini Denmark inatekelezwa na SUA kwa usimamizi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Mkoa wa Morogoro, Dar es salaam na Zanzibar.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: