Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Singa  Kata ya Kinampundu katika ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) aliyoifanya hivi karibuni wilayani Mkalama.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Singa katika ziara hiyo.

Wananchi wakijiji cha Singa  wakicheza ngoma wakati wakimkaribisha Mkuu wa wilaya katika ziara hiyo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mkalama  Lameck Itungi akizungumza katika  ziara hiyo.

Wananchi wa kijiji cha Singa wakiwa kwenye mkutano wa mkuu wa mkoa .

Katibu tawala wa Wilaya ya Mkalama,.Elizabeth Rwegasira akifanya utambulisha kwa watumishi wa Halmashauri pamoja na msafara uliongozana na Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Wataalamu kutoka ngazi ya wilaya na Mkoa  wakisikiliza hotuba ya Mkuu wa Mkoa katika kijiji cha  Mnguli kitongoji cha Kipamba.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Gumanga, James Mkwega akitoa neno la shukrani kwa serikali ya awamu ya sita  kwakutoa fedha za utekelezaji wa miradi kwa wilaya ya Mkalama  ambapo pia amesema  wataunga mkono juhudi za serikali kwa kusimamia fedha za  miradi vizuri pamoja na kufanya kazi kwa bidii kwa masilahi mapana ya wilaya na wananchi wa Mkalama.

Diwani wa Kata ya Mwangeza ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Mkalama, Bosco Samwel akizungumza  kwenye ziara hiyo.

Wananchi wa Kijiji cha Munguli Kitongoji cha Kipamba wakitumbuiza kwa ngoma za asili  za jamii ya Wahadzabe wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa katika  Kijiji  cha Munguli.

Mkutano ukiendelea.

 Afisa Mazingira Wilaya ya Mkalama, Amon Sanga akieleza utekelezaji wa mradi wakurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula unaotekelezwa katika Kata ya Mpambala kwa vijiji vya Nyahaa, Mkiko, Mpambala , Lugongo pamoja na Kata ya Mwangeza  Kijiji cha  Munguli.

Mratibu wa TASAF Wilaya ya Mkalama, Gudluck Mlau akieleza namna mradi wa kunusuru kaya masikini unavyotekelezwa  wilayani  humo.

Mratibu wa Sensa  Wilaya ya Mkalama, Daniel Tesha akieleza maandalizi ya sensa ya watu na makazi  inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu.

Mwenyekiti wa jamii ya Wahadzabe Edward Mashimba akitoa neno la shukrani kwa ujio wa Mkuu wa Mkoa katika Kitongoji cha Kipamba ambapo alisema jamii ya Wahadzabe iko tayari kushiki shughuli  zote zamaendeleo  pamoja na kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi  ifikapo Agost 23 mwaka huu.

  Mkuu wa Mkoa wa  Singida Dkt. Mahenge akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa jamii ya wahadzabe pamoja na wataalamu mbalimbali wakati wa ziara hiyo.


Rachel Joram na Dotto Mwaibale,  Mkalama  


MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt . Binilith mahenge ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutenga kiasi cha sh.2,118,079,899.00 kutoka  kwenye mfuko wa kimataifa wa mazingira katika kutekeleza mradi  wa kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula  katika kata ya Mpambala na Kata ya Mwangeza Kijiji cha Munguli Wilaya ya  Mkalama mkoani Singida

Dkt. Mahenge aliyasema  hayo  katika ziara aliyoifanya  wilayani hapa  ya kutembelea miradi  mbalimbali  ya maendeleo  inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo wa kunusuru Kaya Masikini (TASAF)  katika Kijiji cha  Singa Kata ya Kinampundu na  Kijiji cha Munguli Kitongoji cha Kipamba  Kata ya Mwangeza  na kusema  kukamilika kwa mradi hiyo itatatua changamoto nyingi za wananchi ikiwani pamoja na  kutatua kero za maji, na kutunza mazingira , kuzuia  mmomonyoko  kwenye  maeneo  yanayotekelezwa miradi.

Aidha amewataka wataalamu wa ngazi zote kusimamia vizuri pamoja  kushirikiana kutatua  changamoto  zitakazojitokeza ili kuharakisha maendeleo ya  Wananchi wa wilaya ya mkalama ikiwa ni pamoja na kutatua migogoro mbalimbali iliyopo katika maeneo  ya miradi.

Akitembelea bwawa la kijiji cha  Singa kata ya Kinampundu  liliochimbwa na wanufaika wa mradi wa kunusuru kaya masikini TASAF aliwataka wananchi hao kutumia mradi huo vizuri ili uweze kuwanufaisha kwakuwataka kulima kilimo cha umwagiliaji na kutoruhusu mifugo kuingia na kukanyaga   kujaza mchanga  kwenye  mradi ili maji hayo yaweze kudumu  hadi kipindi cha masika.

Awali akimkaribisha  Mkuu wa Mkoa wa Singida Mkuu wa Wilaya ya Mkalama  Sophia  Kizigo alianza kwa kumshukuru Mkuu wa Mkoa kutembelea wilaya ya mkalama  kujionea maendeleo ya wilaya  na kuongeza kuwa  ziara yake inachochea kasi ya maendeleo kwani wananchi wanajisikia furaha kutembelewa na viongozi wa kubwa huku akimuomba Mkuu wa  mkoa Dkt . Mahenge inapotokea kugawanywa maeneo ya utawala na Kata ya Mwangeza iangaliwe kwa jicho la pekee kwani ni kubwa hivyo kupunguza ufanisi wa kuwafikia wananchi waliopo maeneo ya mbali.

Diwani wa Kata ya Mwangeza  Bosco  Samwel  aliongeza kuwa ni kweli Serikali imefanya mambo makubwa katika kata yake na hasa kwa jamii ya Wahadzabe inayoishi  kijiji cha Munguli kitongoji cha Kipamba  lakini kilio  bado kipo kwenye ubovu wa miundo mbinu ya barabara , umeme, ukosefu wa  nyumba za walimu pamoja na uhaba wawalimu katika shule shikizi ya Kipamba ambayo tayari imesajiliwa pamoja na shule shikizi ya Mwasulagi ambayo hakuna barabara ya kufika katika shule hiyo.

Afisa Mazingira Wilaya ya Mkalama  Amon Sanga alieleza utekelezaji wa mradi wa mazingira umesaidia kuwepo kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi  kwa vijiji vitano vinavyotekeleza mradi wa LDFS ,huku vikundi vya uzalishaji kiuchumi vikianza kunufaika na ufugaji kwa kupata mizinga ya nyuki  420 pamoja na kuwepo kwa msitu ambao tayari una hati miliki ya kimila unaotoa manufaa  mbalimbali  ikiwa ni pamoja na ufugaji wa nyuki, upatikanaji wa mahitaji ya  jamii ya kihadzabe kama vile dawa,mizizi , matunda na wanyama pori.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa TASAF Mratibu wa TASAF Wilaya ya Mkalma, Gudluck Mlau alisema kuwa kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Mei  2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama im epokea kiasi cha Tsh,.1,591,881,600.00 na malipo yamefanyika katika vijiji vyote 70 ambapo jumla ya walengwa 7,235 walinufaika na mradi huo huku kijiji cha Munguli kikipokea  fedha za ruzuku  kiasi cha Tsh.43,998,000.00 kwa kipindi cha mwezi  Januari  hadi Mei 2022 huku walengwa 354 wakipokea ruzuku zao kwa njia ya mtandao jambo linalowapa urahisi  wakupokea fedha zao .

Sanjari na hayo  Mratibu wa Sensa Wilaya ya Mkalama, Daniel Tesha  alieleza maandalizi ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu kuwa yanaendelea vizuri na kuongeza kuwa  tayari  hamasa imeshafanyika kwa vijiji vyote70 vya wilaya ya Mkalama na tayari eneo  Maalumu limetengwa katika kitongoji cha Kipamba kijiji cha Munguli  maalumu kwa jamii ya wahadzabe na bajeti maalumu  imewasilishwa ofisi ya Takwimu taifa  ili jamii hiyo iweze kupata chakula katika siku hiyo ya sensa na kuweza kushiriki kikamilifu.

Baadhi ya wananchi wajamii ya wahadzabe wameishukuru serikali kuweka kipaumbele na kupeleka miradi mingi katika jamii hiyo huku wakiaahidi kuunga mkono  juhudi za serikali kwa kufanya kazi kwa bidii na kushiriki zoezi la sensa  ya watu na makazi ifikapo Agosti 23 mwaka huu.


Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: