Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amemhimiza mkandarasi anayesimamia ujenzi wa Barabara ya Tanga-Pangani kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Km 50, kuzingatia viwango vyote vya ubora katika kukamilisha barabara hiyo ili iendane na fedha za Watanzania zilizotolewa kwa ajili hiyo.
 
Amesema barabara hiyo ni muhimu kwenye mfumo wa barabara za kitaifa na kimataifa si tu kwa ajili ya Tanga, kwani inaenda kuunganisha na Kenya.
 
Malima alisema hayo wakati akikagua barabara hiyo na nyingine za mkoa huo zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura).

“Kimsingi barabara hii inapunguza zaidi ya Km 120, inafupisha mtandao mzima wa kwenda hadi Mombasa (Kenya) kwa sababu matarajio ni babarabara hii kuingia hadi kwenye mtandao wa Afrika Mashariki.
 
“Kwa hiyo kukamilika kwa barabara hii ni muhimu sana lakini kwa bahati mbaya barabara hii imechelewa kwa sababu mbalimbali kwani ilikuwa Km hizo 50 ilikuwa zimalizike  Novemba mwaka jana lakini hapo katikati ikaingia corona, matatizo ya fidia kwa upande wa Tanga na migogoro mingine kwa hiyo ikachelewa ikapelekwa hadi Desemba mwaka huu,” alisema Malima.
 
Aidha, aliongeza kuwa bado inaonekana kwa asilimia zilizofikiwa maeneo ya lami yanaweza kufikiwa kama Km 30 hadi kufikia Desemba lakini kwa sasa tunaona kasi inakwenda vizuri zaidi kuliko ilivyokuwa kabla.
 
“Kwa hiyo niishukuru serikali kwani miezi kama sita iliyopita tulikuja kukagua na Waziri Mbarawa (Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi – Profesa Makame Mbarawa) tuliweka mkataba usio na maandishi baina ya serikali, Mkoa wa Tanga na wizara kwamba na sisi tutakuwa na utaratibu wa kupita na kukagua maendeleo ya pamoja na wahandisi wa mkoa, Tanroads, Kamati ya Usalama ya Mkoa na pale ambapo tunaona kuna ucheleweshaji wa jambo moja au jingine basi tutatumia fursa hiyo kumwambia waziri kwamba jamani kule barabara yetu mliyotuachia tufanye uangalizi na usimamizi kuna haya na haya.
 
“Hatua hii inatusaidia kujadili barabara ambazo tumeziona kwa macho katika Kikao cha Bodi ya Barabara na wakati tunapokea taarifa ya Tanroads na Tarura mkoa tunakuwa na uelewa wa barabara hizo kwa hiyo wakisema pale daraja sijui limefanya nini tunasema hapana tumeiona.
 
“Kwa mfano kama sasa msimamizi anakwamishwa kwa sababu kuna fedha zimechelewa kidogo kama bilioni tisa hivi ambazo zinamuweka kwenye hali ya kuchelewesha kazi na kupata kisingizio. Kwa hiyo changamoto zilizopo hapa tumeziona na tumepata taarifa kutoka kwa wahandisi,” alisema Malima.
 
 
Kwa upande wake Meneja wa Tanroads Mkoa wa Tanga, Mhandisi Eliazary Rweikiza alisema mradi huo unaosimamiwa na Mkandarasi Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Ltd. ya nchini China kwa gharama ya Sh bilioni 67.47 imefikia asilimia 37.6 ya utekelezaji na makubaliano na mkandarasi ni kwamba ikamilike Desemba 5, mwaka huu.
 
Alibainisha kuwa kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kulitokana na changamoto mbalimbali ikiwamo malipo kwani hadi kufikia Mei mwaka huu mkandarasi alikuwa anaidai serikali Sh bilioni 9.64.
 
“Aidha, changamoto za kuchelewa kulipa fidia kwa waliofuatwa na barabara ili kupisha mradi, matakwa ya fidia kutoka kwa wamiliki wa maeneo hayo, mkandarasi kuchelewa kulipwa malipo kwa wakati na upatikanaji wa maeneo mazuri ya changarawe na ugonjwa wa corona ambao ulisababisha wataalamu wa mkandarasi kuchelewa kuwasili eneo la kazi.
 
“Lakini pia mwanzoni mwa mradi mkandarasi alikuwa na meneja wa mradi ambaye alikuwa hajui Kiswahili wala Kiingereza na kusababisha mawasiliano ya kiutendaji kuwa magumu. Changamoto hii kwa sasa haipo kwa kuwa meneja huyo aliondolewa na kuletwa mwingine ambaye anajua Kiingereza na ana ,ipango mizuri ya kazi,” alisema.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: