Na Elizabeth Joseph,Arusha.

Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha wameshauriwa kuwa wazalendo kwa tumia vyombo vyao vya Habari kuandaa makala na vipindi vinavyotangaza Vivutio vya utalii vilivyopo mkoani humo bila kujali maslahi ya kifedha.


Ushauri huo umetolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Mh,Maximilian Iranghe wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa Waandishi wa Habari mkoani humo kuhusu masuala ya Maadili,Jinsia na Usalama mtandaoni yaliyoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Shirika la Internews.


Alisema kuwa waandishi wana nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta ya Utalii ikiwemo wa Mkoa wa Arusha kwakuwa ndio lango la utalii nchini hivyo endapo wataungana pamoja na kuamua kutangaza vivutio vilivyopo wageni mbalimbali watashawishika kuja kuona Vivutio hivyo.


"Wakija wageni kutalii kwenye Mkoa wetu tutapata pesa kwa maana Hotel zitapata wageni,sekta ya usafiri itafaaidika na wengine wote tutafaidika kwa pesa ile..........


"Hata Royal Tour ya Rais wetu Mama Samia imewezesha uchumi wa Mkoa wa Arusha kukua hoteli kubwa za kitalii zimejaa wageni hadi Mwezi wa Nane kumejaa"aliongeza Mstahiki Meya.


Aidha aliwataka wanahabari hao kufuata maadili ya Uandishi kwa kuzingatia sheria na taratibu za Nchi kwa kuepuka kuandika habari zisizo na maadili ili kutojiingiza katika migogoro na serikali pamoja na jamii inayowazunguka.


"Wapo waandishi ambao wanakwambia unataka tuandikaje story yako?unashangaa!,lakini mwisho wa siku anakupiga mzinga,wengine inafika hatua wanakutishia kuwa wana habari yako fulani na kudai chochote ili wasiitoe,nyie niwaombe mzingatie sheria za Nchi na kazi zetu"alieleza Mh, Iranghe.


Awali akimkaribisha Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha Bw, Claud Gwandu alitaja lengo la mafunzo hayo ni kukumbusha wajibu wa waandishi hao katika kazi zao za kila siku hasa katika kuzingatia maadili na sheria za Nchi.


Gwandu pia aliwataka waandishi kujenga mahusiano mazuri na vyanzo vyao vya Habari ikiwa ni pamoja na kuvilinda vyanzo hivyo kwa kutokutoa siri za vyanzo vyao vya habari ili kujenga mahusiano mazuri baina  yao.


Mwisho.

Share To:

Post A Comment: