TAASISI  ya  Bloomberg Media Initiative Africa (BMIA)  imetangaza  kuanza kwa awamu ya pili ya programu ya mafunzo ya uandishi wa habari za fedha (FJT) kwa waandishi wa Tanzania. Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha waandishi wa habari wa fedha na biashara kuandika habari za kina zinazohusu sekta hiyo. 

Awamu hiyo ya pili inafanyika baada ya mafunzo hayo kusimama kwa mikaa miwili kutokana na changamoto za ugonjwa wa Covid-19.

Mafunzo hayo yanaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Shule Kuu ya Biashara ya Strathmore(Strathmore Business School), Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (University of Dar es Salaam Business School)  na Shule Kuu ya Habari na Mawasiliano ya Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (University of Dar es Salaam School of Journalism and Mass Communication). Kurejewa kwa mafunzo hayo kunatokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika awamu ya kwanza iliyofanyika 2019 ambapo waandishi wa habari 40 walipata taaluma mbalimbali kuhusiana na uandishi wa habari za fedha na biashara.

 Katika awamu ya pili kutakuwa na waandishi wa habari 50 kutoka vyombo vya serikali, sekta binafsi,taasisi zisizokuwa za kiserikali na vyombo vikubwa vya habari. Imeelezwa kuwa mafunzo hayo ya miezi sita yatazingatia mada mbalimbali zikiwamo uchambuzi wa data,soko la hisa, uhasibu,sera, uchumi na hivyo kuwezesha mabadiliko ndani ya vyombo vya habari ya namna ya kuandika habari za fedha na biashara.

 Mafunzo hayo yatatolewa na waandishi wa habari wa Bloomberg News na shule zilizotajwa.

 Mafunzo kuhusu uandishi wa habari za fedha na biashara nchini Tanzania yamelenga kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwajibikaji, uwazi na utawala bora. Mafunzo hayo ni sehemu muhimu  na ya msingi kwa BMIA kuchangia maendeleo katika uandishi wa habari za fedha na biashara barani Afrika, kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari katika kuleta uwazi, uwajibikaji na utawala bora.

 Akizungumzia taarifa hiyo Mkurugenzi  BMIA, Erana Stennett, anasema: “Tumefurahishwa na kurejea tena katika kutoa mafunzo ya programu baada ya miaka miwili. Tunaamini kwa kuwapa waandishi wa habari ujuzi na maarifa ili kuripoti vyema masuala ya biashara na fedha tunachangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Tanzania.”

 


Akizungumza katika uzinduzi huo, Gavana wa Benki Kuu (BoT) Profesa Florens Luoga alisema: “Katika kipindi hiki kigumu baada ya janga la corona, uandishi thabiti wa habari za kibiashara na kiuchumi ni msingi mkubwa wa kuweza kuwafahamisha wadau ili kuweza kuwa na msukumo mkubwa wa ukuaji wa uchumi. Kwa kutoa mafunzo kwa wanahabari zaidi, BMIA inachangia maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania.”

 Kuzinduliwa kwa awamu ya pili nchini Tanzania kunafuatia kuwapo kwa mafanikio makubwa ya programu hiyo kwa nchi za Kenya, Nigeria, Afrika Kusini, Ghana, Zambia, Côte d’Ivoire na Senegal, ambapo zaidi ya waandishi 600 wamekamilisha mafunzo hayo. 

 Tangu kuzinduliwa kwa programu hiyo mwaka 2014, BMIA imewafikia wadau 1,000 barani Afrika. BMIA pia imedhamini mikutano minne iliyokutanisha wamiliki wa vyombo vya habari na viongozi waandamizi mkatika masuala ya biashara, serikali na vyama vya kiraia.

 

Share To:

Post A Comment: