Na Joachim Nyambo,Mbeya.


 


SERIKALI mkoani Mbeya imesema zaidi ya watoto 70 wanashikiliwa na polisi mkoani humo kutokana na oparesheni maalumu iliyofanywa jijini Mbeya ikilenga kuwakamata watoto wanaoishi katika mazingira yasiyo rasmi na yanayotajwa kuwa chanzo cha kuzalisha wahalifu wanaohatarisha amani ndani ya jamii.


 


Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Mbeya,Juma Homera ambaye ndiye Mkuu wa mkoa huo,miongoni mwa wanaoshikiliwa ni pamoja na watoto walio katika umri mdogo ikiwemo miaka saba au nane.


 


Watoto walio na umri wa miaka saba na pia minane ni sehemu ya watoto waliopo kwenye kundi linalotambuliwa na Programu ya Kitaifa ya miaka mitano ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) iliyozinduliwa mwaka jana ikilenga kuyaangazia maisha ya watoto walio katika umri wa miaka sifuri had inane katika Vipengele vya malezi jumuishi ikiwemo Afya bora,Lishe bora,Ulinzi na usalama,Fursa za ujifunzaji wa awali na malezi yenye mwitikio.


 


Homera amebainisha kukamatwa kwa watoto hao zaidi ya 70 katika kikao chake na waandishi wa habari kilichofanyika mapema leo kilicholenga kuzungumzia maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya kimataifa ya Familia yatakayofanyika Mei 15 mwaka huu.


 


Mkuu huyo wa mkoa amesema miongoni mwa watoto waliokamatwa wapo waliotelekezwa na wazazi au walezi wao na pia wapo waliokimbia familia zao kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ugumu wa maisha kutokana na hali duni za kiuchumi na pia baadhi kufanyiwa ukatili.


 


Amefafanua lengo la oparesheni hiyo ni kuwa ni mwelekeo wa siku ya familia duniani uendane na juhudi za kuwarejesha watoto majumbani kwao ili waweze kujumuika na familia zao na kuadhimisha siku hiyo kwa pamoja.


 


“Jana tumefanya oparesheni hapa mjini zaidi ya watoto 70 tumewakamata baadhi yao hawana baba wala mama na wengine wana mzazi mmoja..watoto hao mpaka hivi sasa wako pale mahabusu  tunawatafuta wazazi wao.”


 


Amewasihi wakazi katika wilaya za mkoa wa Mbeya na maeneo ya jirani kufika katika mahabusu zilizopo kwenye vituo mbalimbali vya polisi vilivyopo mkoani hapa kwaajili ya kuwatambua na kuwachukua watoto.

Amesisitiza kuwa watoto wanaoachwa kuzurula na kuishi mitaani kwenye makazi yasiyo rasmi ndiyo baadaye hugeuka na kuwa wahalifu baada ya kukutana na kujiunga na makundi ya vijana walio na tabia hizo ambao hupenda kuwatumia kutokana na umri wao mdogo.

“Tunashauri na kupendekeza wazazi waje wachukue watoto wao..watoto hao ndiyo baadaye wanageuka kuwa panya road..wanageuka kuwa nyuki..wanageuka kuwa watukutu kwenye maeneo mbalimbali na walio wengi  wana miaka saba,nane,tisa,kumi  mpaka kumi na tano.”


Mkuu huyo wa mkoa amesema oparesheni hiyo itakuwa endelevu ili kuhakikisha watoto wote wanaozurula mtaani wanakamatwa kwakuwa tayari athari mbaya za uwepo wao zimeanza kuonekana kwa baadhi yao kujihusisha na vitendo vya udokozi kwenye magari.


 


“Baada ya kuwakamata tunafanya tathmini ili kujua kwao ni wapi wazazi wao wako wapi na kasha ufanyike utaratibu wa kuwarudisha walikotoka.” Aliongeza


Mtandao wa Wanahabari vinara wa masuala ya watoto uliotapakaa katika mikoa yote ya Tanzania bara chini ya Mwamvuli wa Muungano wa vyama vya waandishi wa habari nchini(UTPC) kwa ufadhili wa Shirika la Children in Crossfire(CiC) wamekuwa wakipambania vipengele vya MMMAM kwa kuandika habari zenye kuleta uchechemuzi kwa jamii ili kuboresha maisha ya watoto walio na umri wa kuanzia miaka sifuri hadi nane

Share To:

Post A Comment: