Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Sophia Kizigo, akizungumza na Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Sensa Wilaya ya Ikungi cha maandalizi ya uhabarisho wa zoezi la Sensa  linalotarajia kufanyika mwaka huu kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro.

Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi wa wilaya hiyo Faraja Maliga akizungumza kwenye kikao hicho.

Mratibu wa Vikao wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Peter Bahati akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Mjumbe wa kikao hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga akizungumza kwenye kikao hicho.

Wajumbe wakiwa kwenye kikao hicho.
Mjumbe wa kikao hicho ambaye pia ni Afisa Elimu wa Wilaya hiyo, Magreth Kapolesya akizungumza kwenye kikao hicho.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Justice Kijazi ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo akichangia jambo kwenye kikao hicho.

Kikao kikiendelea.

Wajumbe wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.



Na Dotto Mwaibale, Ikungi


MKUU wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Sophia Kizigo,ameagiza watendaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kuitisha mikutano ya wananchi ili kuwajulisha waweze kuchangamkia fursa ya ajira za muda za makarani na wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi zilizotangazwa na serikali.

Alitoa agizo hilo kwenye kikao cha maandalizi ya uhabarisho wa zoezi la Sensa  linalotarajia kufanyika mwaka huu wakati akizungumza na wajumbe wa kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro.

"Nawaombeni waelekezeni watendaji wa vijiji na vitongoji waitishe mikutano ya hadhara ya kuwajulisha wananchi kuhusu ajira fupi za makarani na wasimamizi wa zoezi la Sensa ili kila mtu ajue na mwenye sifa achangamkie fursa hiyo jambo litakalo saidia kuondoa malalamiko ya kusema hatukuambiwa au hatukupata taarifa" alisema Kizigo.

Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi wa wilaya hiyo Faraja Maliga alisema hivi karibuni, Nchi yetu ya Tanzania inatarajia kufanya zoezi la Sensa ya watu na makazi Agosti 23/ 2022, na kuwa zoezi hilo litahusu ukusanyaji wa taarifa za kila mtu aliyelala ndani ya mipaka ya nchi usiku wa kuamkia siku ya Sensa yaani Agosti 23/2022.

Alisema lengo la sensa  ya watu na makazi ni kupata taarifa sahihi za kidemografia, Kijamii, Kiuchumi na hali ya Mazingira kwa lengo la kupata Takwimu sahihi zitakazoiwezesha Serikali na wadau wengine kupanga kwa usahihi  mipango ya maendeleo ya watu wake katika sekta mbalilimbali za elimu, afya, hali ya ajira, miundombinu kama barabara , Nishati na maji safi, Kwa msingi huo, Sensa ni zoezi muhimu ambalo kila mmoja kwa nafasi yake analazimika kushiriki na kutimiza wajibu wake ili kuhakikisha  inakuwa ya Mafanikio Makubwa .Hii itasaidia Serikali  kutimiza wajibu wake kwa Wananchi kulingana na idadi  ya watu ya eneo husika ikiwa kama msingi mkubwa wa ugawaji wa keki ya Taifa kwa kila eneo la utawala hapa nchini.

Alisema kwa upande wa Wilaya ya Ikungi zoezi hilo litahusu ukusanyaji wa taarifa hizo kwa kila mtu aliyelala ndani ya mipaka ya wilaya hiyo.

"Zoezi la ukusanyaji wa taarifa hizi litafanywa kwa kutumia Makarani wa Sensa ambao watatembelea kaya zote ndani ya Wilaya na kufanya mahojiano ya ana kwa ana baina ya karani wa Sensa na mkuu wa kaya na kama mkuu wa kaya hatakuwepo karani wa  Sensa atafanya mahojiano na mtu mzima yeyote katika kaya ambaye ana taarifa za kutosha kuhusu kaya na watu wote waliolala katika kaya husika usiku wa kuamkia siku ya sensa' alisema.

Aliongeza kuwa watu watakaohesabiwa ni watu wote watakaolala katika kaya binafsi pamoja na watu wote watakao kuwa katika kaya za wageni,Hospitali,Magereza,Mabweni ya Wanafunzi,Kambi za jeshi,Vituo vya kulelea watu wenye Mahitaji Maalumu kama vile Wazee na watoto yatima,kambi za wavuvi,watu wasio na makazi maalumu na vituo vya usafiri wa umma (Vituo vya mabasi, gari moshi,Viwanja vya ndege na bandarini).

Alisema katika kila kitongoji kutakuwa na watu watatu watakaohusika na zoezi la sensa ambao ni Karani wa sensa, Msimamizi wa maudhui na Msimamizi wa TEHAMA wakiongozwa na Mwenyekiti wa kitongoji husika ambao watatembelea kila kaya na kuchukua taarifa za kila mtu aliyelalala hapo usiku wa kuamkia siku ya sensa.

Alisema kamati za sensa za Vitongoji, Vijiji na Kata ndio wasimamizi wa zoezi la sensa katika Maeneo yao na Kamati ya Sensa ya Watu na makazi ya Wilaya ndiyo Msimamizi wa Shughuli zote za sensa ndani ya Wilaya Ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati hiyo. 

Maliga alizitaja taarifa zitakazoulizwa kuwa zitahusu maeneo ya kidemografia (Umri,Jinsi,Hali ya ndoa) yaani za ulemavu (Aina ya ulemavu na chanzo cha Ulemavu),taarifa za Uhamaji, vitambulisho vya utaifa na uhai wa Wazazi,elimu, shughuli za kiuchumi, umiliki wa ardhi na TEHAMA, hali ya uzazi,Taarifa za vifo na vifo vitokanavyo na uzazi, Taarifa za nyumba, hali ya umiliki wa nyumba, vifaa, rasilimali na udhibiti wa mazingira, kilimo,mifugo,uvuvi na mistu,Taarifa kuhusu mpango wa TASAF,majengo/nyumba, Anwani za makazi na huduma za jamii katika ngazi ya kitongoji.

Akizungumzia hali halisi ya utekelezaji wa zoezi la sensa kwa sasa alisema ni kutengwa kwa maeneo ya kuhesabia na kuwa zoezi la kuhesabu watu litafanyika katika ngazi ya kitongoji na wilaya hiyo ina jumla ya vitongoji 539.

Alitaja utekelezaji mwingine kuwa ni kuundwa kwa Kamati za Sensa,
kamati za sensa za kata, Vijiji na Vitongoji zimeundwa ambapo katika ngazi ya Kata Diwani ndie Mwenyekiti na katibu wake ni Mtendaji wa Kata; katika ngazi ya kijiji Mwenyekiti wa kijiji ndie mwenyekiti wa kamati na katibu wake ni Mtendaji wa kijiji; na katika ngazi ya Kitongoji mwenyekiti wa kamati ya sensa ni mwenyekiti wa kitongoji na katibu wa mwenyekiti wa kitongoji ndiye Katibu wa kamati. 

Alisema kazi nyingine ni  uhamasishaji na utoaji elimu kuhusu sensa ya Watu na makazi ya mwaka 2022, zoezi la uhamasishaji na utoaji elimu kwa wananchi kuhusu sensa limeanza kufanyika na kuwa uhamasishaji unafanyika kwa kutumia njia ya kuwaandikia watendaji wa kata na vijiji wote kuhakikisha kuwa agenda ya sensa inakuwa agenda ya kudumu katika vikao vyote vitakavyofanyika kwenye maeneo yao hadi sensa itakapofanyika, pia wamesambaza vipeperushi vya sensa kwenye ofisi za kata, vijiji na mashuleni ili kusaidia kufikisha ujumbe kwa wananchi, kwa kutumia mitandao ya kijamii.

" Aidha katika baadhi ya maeneo tulifika na kuelimisha wananchi ambao tulifanikiwa kukutana nao na kuwa katika kikao cha Baraza la madiwani kinachotarajiwa kufanyika wiki hii tumealika viongozi wa makundi mbalimbali yaani wazee maarufu, viongozi wa dini, viongozi wa taasisi binafsi, wafanya biashara, wanahabari na kiongozi wa machifu na viongozi wa vyama vya siasa lengo likiwa kusaidia kusambaza taarifa kuhusu sensa kwa wananchi" alisema Maliga.

Alitaja kazi nyingine kuwa ni kutangaza Ajira za muda za Makarani, Wasimamizi wa Maudhui na Wasimamizi wa TEHAMA. Ili kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi ambap, serikali inatarajia kuajiri makarani wa sensa, wasimamizi wa maudhui na wasimamizi wa TEHAMA ambao watapita katika kaya ndani ya kitongoji kwa ajili ya kuchukua taarifa za kila mtu aliyelala katika kaya husika usiku wa kuamkia siku ya sensa. 

Alisema hadi sasa serikali imeshatoa tangazo la ajira hizo na tayari wamelipokea na kusambaza katika kata, vijiji na vitongoji kwa ajili ya kubandikwa kwenye maeneo ya wazi ili watu wote wenye sifa stahiki waweze kuomba nafasi hizo.  Uhamasishaji wa Wananchi Kuhusu kuomba nafasi za ajira hizo unaendelea kwa kutumia Mitandao ya kijamii, kubandika matangazo kwenye maeneo ya wazi wilaya nzima kwa kutumia Watendaji wa kata na vijiji, Walimu na viongozi wengine wa Taasisi mbalimbali za umma na binafsi pamoja na Timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya mipango ikiongozwa na Mratibu wa Sensa kupita maeneo mbalimbali kujiridhisha kama matangazo yamebandikwa na kuendelea kutoa elimu.
Aidha Maliga alitaja kazi ya mwisho walioifanya ni kubaini kaya zote  za jumuiya na kuwazoezi hilo linaendelea na kuzitaja kaya hizo kuwa ni  Vituo vya kulelea watoto yatima au wazee, nyumba za kulala wageni, Maeneo ya wachimbaji madini, Hospitali, kambi za jeshi, mabweni ya wanafunzi, magereza, kambi za wavuvi, vituo vya kusafiria na watu wasiokuwa na makazi maalumu.

Maliga alisema zoezi la sensa ya watu na makazi linahitaji ushirikiano wa kamati zote za sensa kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, kata na Wilaya pamoja na wataalamu. Serikali imeunda kamati hizo kwa lengo la kurahisisha zoezi la usimamizi wa sensa katika kila ngazi. Ili kufanikisha zoezi hili la sensa kwa asilimia 100 ,uhamasishaji na utoaji wa elimu kuhusu sensa ya watu na makazi unahitajika na kuwa ujumbe wa Sensa ya Watu na makazi, 2022  ni  “Sensa kwa Maendeleo, Jiandae kuhesabiwa” 

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: