Na Mwandishi wetu



Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mabula Misungwi Nyanda, amebainisha kuwa changamoto ya uvamizi wa tembo wilaya ya Meatu, Mkoani Simiyu inatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.



Mabula ametoa kauli hiyo Mei 23, 2022 alipofanya ziara ya kikazi katika vijiji vya Mwagila na Malwilo wilayani Meatu.



Katika nyakati tofauti akizungumza na wananchi wa vijiji hivyo, Mabula Kwa niaba ya Serikali ametoa pole za dhati kwa wananchi waliopoteza ndugu zao kwa janga la wanyama tembo na wale waliojeruhiwa na wanyama fisi.



Kaimu Kamishna huyo amesema, suala la migongano baina ya binadamu na wanyamapori (tembo) limekuwa ni janga kubwa nchini na hivyo kuilazimu Serikali kuchukua hatua kadhaa.



Ametaja moja ya hatua kuwa ni uandaaji wa mpango madhubuti wa kutatua changamoto hiyo kwa kujenga jumla ya vituo 11 nchini vya askari wa Uhifadhi kwa ajili ya kuimarisha doria za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo ya vijiji vinavyoathiriwa na wanyama hao ambapo viwili vitajengwa katika Wilaya ya Meatu.



Pia Mabula ameeleza kuwa mpango mkakati wa kitaifa unaosimamia utatuzi wa migongano baina ya watu na wanyamapori (2020 - 2024) unatekelezwa na taasisi zote za Uhifadhi, halmashauri za Wilaya na wadau wengine wa Uhifadhi.



Aidha Mabula Misungwi ametoa wito Kwa wananchi wa vijiji hivyo, kushirikiana na askari wahifadhi katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kwa sababu ulinzi ni jukumu la kila Mtanzania.



Amesema jukumu kubwa la Serikali ni kuwawezesha wananchi Kwa kuwapa elimu ya kujilinda dhidi ya wanyama hao na kuwasogezea huduma karibu ili pale mwananchi anapopiga simu askari wawe karibu.



Nao waheshimiwa madiwani wa kata za Mbugayabanhya, Lingeka na Mwakidandu, kwa nyakati tofauti wameeleza kuwa kata zao zimekuwa zikipata changamoto kubwa, kutokana na wanyama tembo, mbali na juhudi kubwa zinazofanywa na askari wahifadhi.



Madiwani hao wamesema uhaba wa magari ya kutosha na maaskari umekuwa sababu kubwa ya kuongezeka Kwa changamoto za uvamizi katika maeneo yao.



Awali katika maelezo yake, Mkuu wa Wilaya ya Meatu Mhe. Faudhia Hamidu Ngatumbura, ametoa wito kwa wananchi kupenda kutoa taarifa sahihi kwa watu sahihi ili wasaidiwe kwa haraka pale wanapovamiwa na wanyama tembo.



"Changamoto kubwa tunayopata ni utolewaji taarifa za uvamizi zisizo sahihi, kwa watu sahihi, kwa wakati sahihi..zinatusumbua.



"Hebu tunapozisikia hizi taarifa au tunapoona kundi la tembo tutoe hapa, amesema Kamishna hapa Sasa wewe unampigia mtu aliyepo Dodoma, unamuacha aliyepo Meatu , utasaidiwaje?" ameongeza.



Ziara ya Kaimu Kamishna Mabula Misungwi imelenga kukagua maeneo ya kujenga vituo vya kudhibiti Wanyamapori wakali na waharibifu na kutoa pole Kwa wahanga kufuatia changamoto inayoletwa na tembo.


Share To:

Post A Comment: