Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Juma Mkomi akizungumza na Watumishi wa NCAA wakati wa ziara yake Ofisi za Makao makuu ya NCAA Karatu Mkoani Arusha
Menejimeti ya NCAA wakiwa Makini kumsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakati akizungunza na Watumishi wa NCAA
Watumishi wa NCAA wakiwa makini kusikiliza Maelekezo ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii wakati wa ziara yake Makao Makuu ya NCAA yaliyoko Karatu Mkoani Arusha


Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Juma Mkomi amesisitiza watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuendelea kuimarisha shughuli za uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu ili ziendelee kuwa kivutio kwa wageni wanaotembelea hapa Nchini.

Bw. Mkomi ametoa kauli hiyo katika ziara aliyoifanya makao makuu ya ofisi za Hifadhi ya Ngorongoro tarehe 24 Mei, 2022 ambapo alikutana na menejimenti na watumishi wa mamlaka hiyo kwa lengo la kujitambulisha na kukagua shughuli mbalimbali za utendaji kazi.

Ameeleza kuwa sambamba na kuimarisha shughuli za Uhifadhi watumishi wote katika sekta ya maliasili na utalii wanapaswa kuongeza juhudu za utoaji wa huduma bora kwa wageni wengi wanaotarajiwa kuitembelea nchi yetu hasa baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Mhe. Rais kutangaza vivutio vya Utalii na kuhamasisha wawekezaji kupitia Filamu ya The Royal tour.

“Sambamba na kuongeza juhudi za Uhifadhi, tukumbuke kuwa baada ya uzinduzi wa filamu maarufu ya The Royal tour tunategemea kupokea wageni wengi watakaotembelea vivutio vya utalii hivyo lazima kila mtumishi ajiimarishe katika utoaji huduma bora zaidi kwa wageni ili wakirudi kwao wawe mabalozi wazuri wa Nchi yetu”. Alisisitiza Mkomi.

Mkomi amebainisha kuwa pamoja na Sekta ya Utalii kuchangia asilimia 17 ya pato la Taifa bado kuna fursa ya sekta hiyo kuongeza bidii na kuchangia pato la Taifa kwa zaidi ya mara mbili ya kiwango kilichopo sasa.

Naibu Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa nyongeza ya mshahara kwa watumishi kwa asilimia 23.3 na kutoa wito kwa watumishi kuwa wahakikishe ongezeko hilo linaenda sambamba na wajibu wa watumishi kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza mapato zaidi yatakayosaidia Serikali kutekeleza miradi mingine ya wananchi.

Katika hatua Nyingine naibu katibu ameielekeza NCAA kuhakikisha mitambo ya ukarabati wa miundombinu iliyonunuliwa kwa fedha za UVIKO inatunzwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kusaidia uboreshaji wa miundmbinu hasa ya barabara kwa miaka mingi ijayo.

Kwa Upande wake Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt. Christopher Timbuka amemhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa uongozi wa NCAA utaendelea kuongeza jitihada za uhifadhi na Ulinzi wa Wanyamapori sambamba na utoaji wa huduma za mafunzo ya huduma kwa mteja kwa watumishi wake ili kuongeza ufanishi katika kuhudumia wageni wanaotembelea vivutio vya Hifadhi ya Ngorongoro.
Share To:

Post A Comment: