Na. Catherine Mbena /TANAPA.


Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), William Mwakilema amewataka makamishna wapya kufanya kazi kwa weledi, ushirikiano na kufuata utaratibu katika kutekeleza majukumu yao mapya.

Kamishna Mwakilema ameyasema hayo leo   katika Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za  Taifa Tanzania jijini Arusha wakati wa zoezi la kuwavisha vyeo na kuwaapisha makamishna wateule wa Uhifadhi  walioteuliwa na Bodi ya Wadhamini ya shirika hilo kushika nafasi mbalimbali za uongozi.

“Mmeaminiwa na Bodi ya Wadhamini kutekeleza majukumu haya, pale mtakapohitaji usaidizi wetu msisite, tupo tayari wakati wote. Uongozi wa pamoja iwe ndiyo nguzo yenu katika utendaji kazi.” Alisema Mwakilema.

Aidha, Kamishna Mwakilema amewaasa kuwa na umoja, mshikamano, nidhamu na uadilifu pamoja na kufanya kazi kwa bidii hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo ya TANAPA, na miradi ya ufadhili pia  kuhakikisha inakamilika kwa wakati kwa kuzingatia thamani ya fedha za miradi hiyo.

Akishuhudia tukio, hilo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,  Juma Mkomi aliwaasa  watumishi wa TANAPA kuwa na umoja katika utendaji kazi ili kuleta tija iliyokusudiwa pamoja na kuongeza juhudi za kuhifadhi maeneo yote ili juhudi zote zilizofanyika  za kutangaza utalii ziweze kufanikiwa.  

Hivi karibuni Bodi ya Wadhamini ya TANAPA ilifanya uteuzi katika nafasi mbalimbali za uongozi pamoja na upandishwaji vyeo wa viongozi waandamizi wa shirika kwa lengo la kuboresha utendaji kazi ambapo ilimpandisha cheo  Afisa Uhifadhi Mkuu, Richard Shilunga kuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere,

Afisa Uhifadhi Mkuu, Dkt. Emillian Kiwhele alipandishwa cheo kuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Idara ya Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Kanda ya Kaskazini

Afisa Uhifadhi Mkuu, Sonia Lyimo alipandishwa cheo kuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na  Mkuu wa Idara ya Huduma za Shirika Kanda ya Magharibi.

Pia Afisa Uhifadhi Mwandamizi, Salim Mjema alipandishwa cheo kuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Idara ya Huduma za Shirika Kanda ya Kaskazini.Share To:

Post A Comment: