Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ametaka kuharakishwa kwa mpango wa  upatikanaji  wa Mbolea ya Ruzuku kwa wakulima nchini.


Ameyasema hayo leo tarehe 13 Mei, 2022 wakati alipofanya ziara yakutembelea kiwanda cha mbolea ya asili  cha  Itracom kilichopo eneo la Viwanda Nala jijini Dodoma ambacho kinajengwa na mwekezaji kutoka Nchini Burundi ambacho ujenzi wake ulianza mwezi Julai, 2021 na kikitarajiwa kukamilika mwezi Julai 2022 ambapk kwa sasa kimefikia asilimia 80.


Kiwanda hicho kinatarajiwa kuanza uzalishaji wa awali Juni na Julai mwaka huu huku kikitarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 3,000 na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha jumla ya  tani 600,000 za mbolea kwa mwaka baada ya kukamilika, ambapo katika hatua ya awali kitazalisha tani 200,000.


Chongolo ametoa maagizo hayo kwa Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Kilimo kuharakishwa mchakato wa upatikanaji wa ruzuku kwenye mbolea ili kudhibiti upandaji wa bei inayowaumiza wakulima.


Amesema, Rais hivi karibuni aligawa vitendea kazi kwa maofisa ugani na kutoa maelekezo mahsusi ya kutaka Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Kilimo kukaa pamoja Ili kuhakikisha jambo hilo linatekelezeka.


Aidha, Chongolo amesisitiza kuwa ruzuku hiyo inayokwenda kuwekwa katika mbolea ni lazima iwe ni yenye tija na yenye kulinda wawekezaji wa ndani ya nchi.


Aidha wakati huo huo, Chongolo amekemea baadhi ya taasisi na kampuni za serikali zinazohusika kusimamia Mbolea kutokufanya kazi kwa mazoea ambapo amezitaka  kufanya Kazi kwa ushindani kwa kuratibu na kusimamia bei ya mbolea.


Amesema kuwa katika msimu uliopita wakulima walipata changamoto ya upatikanaji wa mbolea, Hali hiyo ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa ugonjwa wa COVID- 19 ambapo mbolea ilikuwa ikigombewa kwenye soko, hivyo bila kusimamiwa sawasawa  inapofika Nchini inapanda  bei zaidi na kuwaumiza wakulima.

Share To:

Post A Comment: