Na;Jusline Marco;Arusha


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Tulia Ackson amesema ukuaji mkubwa wa faida uliopata benki ya CRDB unastahili kuwa mfano wa kuigwa na taasisi zingine za fedha nchini.


Dkt Tulia ametoa pongezi hizo leo jijini Arusha wakati akifungua semina ya elimu ya fedha iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wanahisa wake na Watanzania kwa ujumla wakati wakijiandaa na Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa unaofanyika Mei 22 mwaka huu katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha AICC.


Amesema ukuaji huo umetokana na uwekezaji na usimamizi mzuri katika uendeshaji wa benki hiyo hivyo, kuwawezesha wanahisa kupata gawio ambalo sasa litaongezeka hadi kufikia asilimia 64 kwa hisa.


Dkt Tulia amesema benki hiyo imeendelea kudhihirisha kwa vitendo kuwa Benki kiongozi nchini kwani kila mwaka imekuwa ikitengeneza faida ya uwekezaji kwa wanahisa wake na kuzitaka taasisi nyingine za umma na binafsi kuiga mfano.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi benki hiyo, Dkt Ally Laay amesema wanajivunia kuendelea kukuza thamani ya uwekezaji wa wanahisa wake ikiwamo Serikali ambayo inamiliki asilimia 36 ya hisa.

Share To:

JUSLINE

Post A Comment: