Na Ahmed Mahmoud

Serikali kupitiaWizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kudhibiti migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika maeneo ya kinga ya hifadhi na maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori Mkoani Simiyu.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo Aprili 5, 2022 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Minza Simon Mjika, aliyetaka kujua mipango ya Serikali ya kudhibiti na kutoa fidia kwa wananchi wa mkoa wa Simiyu.


“Wizara hufanya doria za mara kwa mara kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu na pia vituo viwili vya askari vitajengwa katika maeneo ya Busega na Meatu” Mhe. Masanja. amesema.


Ameongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo Wizara itaajiri askari 600 ambapo kwa sasa maombi ya vibali vya kuajiri yamewasilishwa kwenye mamlaka husika.


Aidha amesema Wizara hutoa mafunzo ya mbinu za kujilinda na kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu ambapo Jumla ya Halmashauri za wilaya 17 zimepatiwa mafunzo.


Pia, Wizara imetoa namba maalum za simu kwenye kila kanda za kiutendaji ili kuwezesha wananchi kutoa taarifa za matukio ya wanyamapori bila malipo.


Kuhusu kifuta jasho na kifuta machozi Serikali imetoa jumla ya Shilingi 790,721,500 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa wananchi 3,598 na kwa upande wa Mkoa wa Simiyu Wizara inafanya uhakiki wa maombi yaliyoletwa ili waanze kulipwa.


Amesema lengo la kifuta jasho/machozi ni kupunguza makali ya madhara ya wanyamapori kwa wananchi na kuwezesha wananchi kuwa mtazamo chanya juu ya uhifadhi na siyo kulipa fidia.


 Serikali inatambua kuwa siyo rahisi kufidia uhai wa binadamu bali inawafariji waathika kutokana na madhara waliyoyapata.Utekelezaji huo ni kwa mujibu wa Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori wa mwaka 2020/2021 – 2024/2025.

Share To:

Arusha Newsroom

Post A Comment: