p>
Mkuu wa Mkoa Singida Dk.Binilith Mahenge akizungumza na Wananchi wa Kata ya Kitaraka wakati alipokuwa katika ziara ya kukagua ujenzi wa Sekondari Mpya ya kata wilayani Itigi mkoani hapa leo ambapo pia alikagua zoezi la Anwani za makazi na postikodi.


Mkuu wa Wilaya ya Itigi Rahabu Mwagisa akizungumza na wananchi hao wakati wa ukaguzi huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, John Mgalula akizungumza katika mkutano huo.
Mkuu wa Mkoa Singida Dk.Binilith Mahenge akizungumza na Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Maria Lyimo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa shule hiyo.
Diwani wa Kata ya Kitaraka, John Subert akiishukuru Serikali kwa kuwajengea shule hiyo ambayo itawaondolea adha watoto wa kata hiyo waliokuwa wakiipata ya kutembea umbali mrefu kwenda katika shule zilizokuwa nje ya kata hiyo ambapo pia alimuomba mkuu wa mkoa kuwasaidia kupata kisima cha maji.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge akizungumza na wasisimazi wa zoezi la Anwani za makazi na postikodi wa Wilaya ya Itigi baada ya kupokea taarifa ya zoezi hilo.
Mratibu wa zoezi la utekelezaji wa operesheni ya Anwani za makazi wilayani humo, Abraham Mpimwi akitoa taarifa ya zoezi hilo kwa mkuu wa mkoa.
Mkazi wa Kata ya Kitaraka Emmanuel Mathias akiiomba Serikali kuwajengea Zahanati ili kuwapunguzia adha ya wananchi ya kufata huduma ya matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Itigi ambapo alijibiwa kuwa tayari zimepokelewa fedha za ujenzi wa zahanati hiyo.
Muonekano wa baadhi ya majengo ya shule hiyo inayoendelea kujengwa.
Wananchi wa kata hiyo wakishiriki kubeba kifusi kwa ajili ya kuweka ndani ya majengo ya shule hiyo.
Ubebaji wa kifusi ukiendelea.
Wananchi wakimsikiliza mkuu wa mkoa (hayupo pichani)
Mkutano na mkuu wa mkoa ukiendelea.
Ukaguzi wa ujenzi wa shule hiyo ukiendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge akiwaangalia mafundi wakati wakiendelea na ujenzi wa shule hiyo.
Baadhi ya watumishi wa Wilaya ya Itigi wanaosimamia zoezi la Anwani za Makazi wakiwa kwenye kikao na mkuu wa mkoa cha kupokea taarifa ya zoezi hilo.
Kikao cha kutoa taarifa ya Anwani za Makazi kikiendelea.
Mhandisi wa Wilaya ya Itigi,  Sembua Mrisha akimuelekeza jambo mkuu wa mkoa wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa jengo la utawala la shule hiyo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Itigi ambaye anasimamia ujenzi wa Sekondari ya Kitaraka, Jacob Mwabeza akitoa taarifa ya ujenzi wa shule hiyo.




Na Dotto Mwaibale, Itigi


MKUU wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge amesema zoezi la Anwani za makazi na postikodi ni la kufa na kupona kutokana na umuhimu wake hapa nchini.

Dk.Mahenge ameyasema hayo  baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa operesheni ya anwani za makazi na postikodi katika ziara ya kukagua zoezi hilo aliyoifanya leo Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.

" Mkurugenzi, Mkuu wa wilaya na timu yenu hakikisheni zoezi ili linakamilika kabla ya Aprili 28 ambapo tutakuwa na kikao cha mkoa kujadili kazi yote iliyofanyika kwa mkoa mzima" alisema Mahenge.

Dk.Mahenge alisema hakuna namna nyingine zaidi ya kukamilisha zoezi hilo kama alivyoagiza Rais Samia Suluhu Hassan na kuamini kazi hiyo ifanyike katika ngazi ya mikoa, wilaya na kuwa hawapaswi kumuangusha.

"Kazi hii ni ya kwetu hivyo mkurugenzi na watu wako wanaofanya kazi vizuri mjue ni kazi ya kufa na kupona hivyo  kwa ujanja na mbinu ya namna yoyote ni lazima ikamilike na kusiwe na sababu nyingine" alisema Mahenge.

Akizungumzia utengenezaji wa vibao vya mitaa alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, John Mgalula  kuwasiliana na wenzake wa mikoa mingine na wadau wengine waliopo mkoani hapa ili kupata bei rafiki itakayosaidia kupunguza gharama kubwa na kufanikisha zoezi hilo.

Mkuu wa Wilaya hiyo Rahabu Mwagisa akitoa taarifa ya  operesheni hiyo ya anwani za makazi alisema mpaka sasa halmashauri hiyo imekusanya taarifa za majengo 30,789 ambapo utekelezaji wake ni asilimia 88 ya malengo ya anwani 35,000.

Alisema jumla ya majina ya Barabara-Vitongoji 489 yamesajiliwa katika mfumo wa Napa na jumla ya vitongoji 133 vimemaliza ukusanyaji taarifa na vitongoji 38 vipo katika hatua za umaliziaji.

Akikagua ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Kitaraka ambayo ujenzi wake utagharimu Sh. 470 Milioni Mahenge aliwapongeza viongozi wa wilaya hiyo kwa kutekeleza mradi huo kwa kuahinisha matumizi ya fedha hizo vizuri tofauti na maeneo mengine aliyokagua miradi ya namna hiyo huku akiwashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kujitoa kwao katika shughuli za maendeleo.

Dk.Mahenge alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kuanzia Sekta ya Afya, Maji, Barabara na Elimu ambapo kwa Mkoa wa Singida kwa kipindi cha mwaka mmoja ametoa Sh.232 Bilioni.

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: