Na Mwandishi Wetu

April 28, 2022 Kampuni namba moja nchini Tanzania kwa utoaji wa huduma za Kidigitali nchini, Tigo Tanzania imeibuka mshindi wa Tuzo ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi iliyotolewa na wakala wa usalama na Afya mahala pa kazi ( OSHA ) katika maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Duniani yaliyofanyika kitaifa katika eneo la Jakaya Kikwete Convention Centre, Jijini Dodoma, yakiwa na Kauli mbiu ya " Act Together to build Health and Safety Culture ",  Tuzo waliyokabidhiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako.

Aidha Prof. Ndalichako amewataka waajiri na wafanyazi kushirikiana pamoja kujenga utamaduni bora wa kuweka mazingira yenye usalama na afya ili kuzuia vihatarishi katika maeneo ya kazi.

Waziri Ndalichako alieleza kuwa, Waajiri na wamiliki wa sehemu za kazi katika maeneo mengi hudhani kuweka mazingira ya kazi salama ni gharama za ziada kutokana na ukosefu wa ufahamu wa faida za kuboresha mazingira ya kazi ili waweze kutambua hasara zinazoweza kutokea hususan inapotokea ajali au ugonjwa katika sehemu ya kazi.

“Ni utamaduni unaohitaji kuona Serikali, Waajiri na Wafanyakazi wanashiriki kikamilifu katika kuweka mazingira salama ya kufanya kazi kupitia mfumo wa haki na wajibu ulioainishwa, ambapo kanuni ya kuzuia vihatarishi inapewa kipaumbele cha juu zaidi,” alieleza Waziri Ndalichako

Kwa upande wake Meneja wa Usalama , Afya na Mazingira kutoka Tigo Bw. Nashon Mdalla amewapongeza wakala wa usalama na Afya mahala pa kazi ( OSHA ) kwa kuwatunuku tuzo hii mara mbili mfululizo mwaka jana  na mwaka huu 2022 .

" Tigo tunatambua umuhimu wa usalama na afya mahala pa kazi mara zote , hivyo basi tumefanya tathmini ya usalama wa wafanyakazi wetu mahala pa kazi ili kuendelea kutoa huduma na bidhaa bora kwa wateja wetu siku zote . Tunahakikisha , kuelimisha na kuhamasisha masuala ya usalama na afya mahala pa kazi pamoja kwa kuweka mifumo thabiti itakayozuia ajali kwa kuchukua tahadhari mapema" . Alimalizia Bwn. Nashon Mdalla.


Share To:

Adery Masta

Post A Comment: