Ikiwa ni sehemu ya hatua na mikakati mbalimbali anayotekeleza kukuza na kuimarisha uchumi na ustawi wa Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, leo anatarajiwa kuandika historia nyingine kwa kutangaza duniani kote, maliasili za utalii na fursa nyingine za biashara na uwekezaji zilizoko Tanzania, atakapoongoza uzinduzi wa Makala ya runinga ya Tanzania: The Royal Tour, huko New York, nchini Marekani.

Uzinduzi wa Makala hiyo Tanzania: The Royal Tour, ambayo ilirekodiwa hapa nchini kati ya mwezi Agosti na Septemba mwaka jana, ni sehemu nyingine ya juhudi za Rais Samia katika kutangaza vivutio vya asili, utamaduni, utalii na fursa za uwekezaji na biashara ambazo Tanzania imebarikiwa kipekee kuwa navyo na vingine havipatikani sehemu nyingine duniani isipokuwa hapa kwetu pekee.

Kupitia Makala ya Tanzania: The Royal Tour, ambayo mhusika mkuu ni Rais mwenyewe, Mheshimiwa Samia, akiwa katika mavazi ya safari, watazamaji dunia nzima, watapata fursa ya kuona kwa kifupi na kwa mbali, akiwaonesha urithi, mandhari na taswira ya kipekee ya utajiri wa kihistoria uliotawanyika kila kona ya maeneo mbalimbali nchini, unaoweza kugawanywa katika makundi matatu - maliasili, utamaduni na rasilimali zilizotengenezwa na binadamu – kuanzia hifadhi za taifa, mbuga, misitu ya asili, fukwe za asili, mapori ya akiba, maeneo ya uwindaji wa kitalii, maporomoko ya mito, mbali ya masalia ya mtu wa kale, pia kuna mabaki ya makazi ya kale (Mji Mkongwe - Zanzibar, Kaole - Bagamoyo, Kilwa n.k) na nyingine nyingi.

Watajionea utajiri wetu kuanzia Zanzibar, Ngorongoro, Serengeti, Olduvai Gorge, Mlima Kilimanjaro, Mikumi, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na Pori la Akiba la Selous, maeneo maarufu ya utalii wa Pwani wa Bahari ya Hindi, uvuvi bora katika Visiwa vya Mafia na Pemba.

Wataona pia urithi wa utamaduni na sanaa, ambao unajumuisha shughuli na maisha ya makabila mbalimbali wakiwemo Wamasai, Wasukuma, Wamakonde na wengine wote, bila kusahau maisha ya Waswahili katika Pwani ya Bahari ya Hindi.

Halikadhalika fursa za kipekee za biashara na uwekezaji katika sekta za kilimo, nishati na madini(kama Tanzanite) bila kusahau ukarimu wa Watanzania, nazo zitatangazwa dunia nzima.

Ni wazi mkakati huu utawavutia watalii na wawekezaji wengi zaidi kuja kufuatilia na kujionea vivutio hivyo na fursa hizo hapa Tanzania, kwa ukaribu na macho yao wenyewe.

Chama Cha Mapinduzi kinatumia fursa hii kumpongeza, kuendelea kumtia moyo na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia kwa namna anavyoendelea kuweka mikakati mbalimbali, kuitafsiri kwa vitendo Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025, ambayo katika Sura ya Pili, kuanzia ukurasa wa 9 – 111, imezungumza na kuwaahidi Watanzania masuala mengi katika eneo la Mapinduzi ya Uchumi kwa Maendeleo ya Watu, kupitia mikakati mbalimbali kama huu wa Makala ya Tanzani: The Royal Tour.

Kupitia eneo la maliasili, utalii na hali yetu ya kijiografia na maisha, kiliahidi kutengeneza ajira, kuongeza watalii, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja, kuongeza pato la taifa, kuweka mazingira ya kukuza hali ya uchumi wa mtu, makundi na taifa kwa ujumla. Pia kutangaza mazao ya biashara na fursa za uwekezaji kedekede tunazomiliki Watanzania.

Kupitia taarifa hii, tunatoa wito kwa Watanzania wote nchi nzima na walioko nje ya nchi, kuunga mkono juhudi hizi, ambapo kwa kuanzia tujumuike katika maeneo yetu, popote tutakapokuwa, iwe kwenye sehemu za kazi, magulioni, minadani, vijiweni, maskani, hotelini, wanapoonesha mipira n.k, tufuatilie na kutazama uzinduzi wa makala hiyo leo Jumatatu, Aprili 18, huko New York, Marekani (ambayo itakuwa ni saa 12 za jioni kwa muda wa Tanzania) na tarehe 21 Aprili, 2022 huko Los Angeles (MUDA), huku tukiendelea na maandalizi ya uzinduzi wa hapa nyumbani Tanzania Aprili 28 na baadae Mei 7 huko Zanzibar, mwaka huu.
Share To:

Post A Comment: