Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Suleiman Mwenda akitoa maelekezo kwa wajumbe wa kamati ya Siasa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo wakati wakikagua moja ya caravati linalojengwa katika Barabara ya Maluga Mtaa Saba -Misuna na Mgungia hadi Kaselya wakati kamati hizo zilipokuwa zikikagua  miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake Tarafa ya Shelui wilayani humo jana.
| Mkzi wa Kijiji cha Maluga akiishukuru Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa shule hiyo. | 
Na Dotto Mwaibale, Singida.
MKUU wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Suleiman Mwenda ametoa mwezi
mmoja kwa Wazazi na Walezi wa wanafunzi 16 wa Tarafa ya Shelui ambao hadi sasa
hawajaripoti shuleni baada ya kufaulu darasa la saba kwenda Sekondari kuhakikisha
wanafanya hivyo na atakae kahidi agizo hilo hatua kali zitachukuliwa dhidi
yake.
Mwenda ametoa agizo hilo jana  wakati akiwahutubia  Wananchi wa
Tarafa ya Shelui kwenye mkutano wa hadhara baada ya  kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo 
kumaliza kukagua miradi ya maendeleo iliyopo katika Tarafa hiyo.
"Serikali haiwezi kuvumilia kuona wanafunzi waliofaulu kwenda
kuanza Sekondari hawaendi shuleni licha ya kutumia fedha nyingi ya kuboresha
mazingira bora ya kupata elimu hivyo naagiza kuanzia leo Machi 30, 2022 hadi
ifikapo  Aprili 30, 2022 watoto hao wawe
wamepelekwa kuanza masomo na wazazi watakao kahidi agizo hilo tutawachukulia
hatua kali" alisema Mwenda.
Akizungumzia ukaguzi wa miradi hiyo iliyogharimu zaidi ya Sh.9  Bilioni alisema kamati hizo zilifanya ukaguzi
huo ili kuona nini kimefanyika katika mwaka mmoja wa uongozi wake Rais Samia
Suluhu Hassan ambaye ametoa fedha nyingi 
kwa ajili ya kutekeleza miradi katika Tarafa hiyo ambapo waliridhishwa
na utekelezwaji wake.
Alisema baada ya kuiona walipanga kufanya mkutano huo wa hadhara ili
kuwaeleza wananchi  mafanikio makubwa ya
utekelezaji wa miradi hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu
kuwa madarakani.
Akizungumza kwa nyakati tofauti 
katika ziara hiyo Mwenda alisema miradi hiyo inafanyika ikiwa ni
utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi 
(CCM) na Serikali inawajibu wa kuikagua ili kuona kama
inatekelezwa kwa viwango vinavyo kubalika. 
Alisema  Serikali inatumia fedha
nyingi kuitekeleza akitolea mfano ujenzi wa madarasa yaliyotokana kwa fedha za mradi wa
maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 ambayo
yamewaondolea adha kubwa ya michango wananchi ya kuchangia ujenzi na ununuaji
wa madawati.
Mwenda  alitumia nafasi hiyo
kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo na kuwaomba viongozi
ilipo miradi hiyo kuwahamasisha wananchi wao kuitunza.
Aidha Mwenda aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa vijana
wanaoshiriki katika zoezi la anuani za makazi na postikodi linaloendelea nchi nzima kwa kuwaelekeza majina ya mitaa na mambo mengine yanayohitajika na
akawaomba kufanya hivyo pia katika zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Mwenda aliwapongeza wananchi wa Tarafa hiyo kwa kuitikia katika kilimo
ambapo mazao mengi yanaonekana kustawi ambapo aliwataka kujiadhari na
walanguzi ambao wameanza kupita kwa wakulima kuwashawishi ili wanunue mazao yao yangali shambani kwa bei ya ulanguzi.
Mwenyekiti wa CCM wilaya
hiyo Samuel Ashery aliwaomba wananchi ilipo miradi hiyo kuitunza na akawataka
wakandarasi kuikamilisha kulingana na thamani ya fedha walizopewa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Innocent Msengi
aliwaomba wakandarasi waliopewa kuijenga miradi hiyo kuijenga kwa wakati kama
walivyo kubaliana kwenye mikataba ili wananchi waweze kuanza kuitumia kwa
wakati.
Baadhi ya  miradi iliyokaguliwa
na kamati hizo  ni ujenzi wa shule mpya
ya Sekondari ya Maluga kwa gharama ya Sh.470 Milioni, ujenzi wa  bweni moja kwa ufadhili wa Mamlaka ya Elimu
Tanzania (TEA) katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tumaini aambao  uligharimu Sh.75 Milioni, ukamilishaji wa
Jengo la Zahanati ya Ulemo ambapo walipokea Sh.50 Milioni na ujenzi wa mradi wa
wa vyoo na uwekaji wa miundombinu ya ya maji ndani ya Zahanati ya Misigiri kwa
gharama ya Sh. 25.2 Milioni.
Miradi mingine iliyokaguliwa ni ujenzi wa barabara za Maluga-Mtaa wa
Saba, Mtaa saba- Misuna na Mgungia-Kaselya kwa gharama ya Sh.492,019,500 fedha
zilizotoka Serikali Kuu, ujenzi wa mradi wa nyumba za Watumishi katika Zahanati
ya Shelui kwa gharama ya Sh.90,000,000 ambao unahusisha jengo moja lenye nyumba
tatu za watumishi, ujenzi wa Kituo cha Afya Mtoa ambacho kitagharimu
Sh.400,000,000 na  ukamilishaji wa vyumba
viwili vya maabara Shule ya Sekondari Mtoa.
Mwenda alitaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa mradi wa maji Kijiji cha Wembereambao umetengewa bajeti ya Sh. 356,080,529 na matengenezo ya barabara ya Shelui kwenda Tintigulu.
Post A Comment: