Wa pili kushoto ni msimamizi wa mradi wa shule hiyo Raymond Mutakyahwa
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Bi. Konstansia Buhiye

Na Mbuke Shilagi Kagera.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera Bi. Constansia Buhiye ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari inayojengwa katika mtaa wa Mafumbo kata ya Kashai Manispaa ya Bukoba.


Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo akiwa ameambatana na kamati ya siasa ya mkoa, mwenyekiti huyo amesema kuwa kata ya Kashai ilistahili kuwa na shule nyingine ya sekondari kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu, wakiwamo wenye uhitaji wa kuendelea na elimu ya sekondari.


Akitoa taarifa ya ujenzi wa shule hiyo mpya msimamizi wa mradi wa ujenzi Raymond Mutakyahwa amesema kuwa tayari wamekwishapokea shilingi milion 600 kwa ajili ya ujenzi huo ulioanza Februari 12, 2022.


Mutakyahwa ameongeza kuwa ujenzi huo ni wa madarasa nane, Maabara ya Kemia, Baiolojia, Fizikia, chumba cha Kompyuta, Maktaba, pamoja na matundu 20 ya vyoo, na kwamba wamefikia hatua ya kuezeka.


Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kashai Ramadhan Kambuga amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Moses Machali kwa kushirikiana naye na kuhakikisha linapatikana eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ambayo uwepo wake utawezesha kuwepo kwa ongezeko la idadi ya watoto wanaoendelea na elimu ya sekondari.


"Kulikuwepo na changamoto ya upatikanaji wa eneo, lakini namshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kusimama kidete na kuhakikisha eneo linapatikana, na napendekeza shule hii iitwe kwa jina la Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni hatua moja wapo ya kuenzi jitihaza za Rais wa awamu ya sita, za kuwaletea wananchi maendeleo" amesema Kambunga.
Diwani wa Kata ya Kashai Ramadhani Kambuga akizungumza
Share To:

JUSLINE

Post A Comment: