NGORONGORO


Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari maelezo Bw. Gerson Msigwa amepongeza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro kwa jitihada za uhifadhi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro hali inayovutia watalii wa ndani na nje ya Nchi kutembelea eneo hilo.

Msigwa ametoa kauli hiyo jana wakati wa ziara ya kikazi kutembelea eneo la hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kijifunza shughuli mbalimbali za Uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.

“Nimefurahi kutembelea eneo la Ngorongoro na kuona nchi yetu ilivyobarikiwa kuwa na rasilimali hii muhimu, naipongeza NCAA kwa kazi kubwa ya kuhifadhi vivutio vya eneo hili, naamini uhifadhi endelevu ndio uliosaidia kutunza mvuto na muonekano wa bonde hili  ambalo ni muhimu kwa  wageni wa ndani na nje ya nchi wanaotembelea Ngorongoro na ikolojia nzima ya kuelekea Hifadhi ya Serengeti.”

Msigwa ameongeza kuwa uhifadhi wa eneo la Ngorongoro ni muhimu kwa kuwa ni moja kati ya maajabu saba ya bara la Afrika na ni eneo lenye  historia ya chimbuko la binadadamu wa kale, ugunduzi wa nyayo za binadamu na kuongeza kuwa wananchi wanapaswa  kuunga mkono juhudi za serikali kulitangaza ili kuendelea kuwa kimbilio la wageni wengi ambao mchango wao unaongeza Mapato ya Serikali. 

Amebainisha kuwa pamoja na mtikisiko wa ugonjwa wa Uviko-19  jitihada za Serikali na wadau mbalimbali zimewezesha idadi ya wageni wanaotembelea Tanzania kuendelea kuongezeka na kufikia wastani wa wageni Milioni 1.7 kwa mwaka.

“Idadi ya watalii wa ndani pia  imezidi kuongezeka, tuendelee kuongeza juhudi za kutangaza vivutio vyetu, naamini ongezeko la watalii wa ndani ni hamasha na chachu ya watalii wa nje kuja, kadri tunavyoongeza mapato yatokanayo na utalii tunazidi kuisaidia Serikali kuboresha huduma muhimu kama afya, maji, shule na uboreshaji wa miundombinu ya utalii” 

Katika eneo la Bonde la Ngorongoro Msigwa amefurahishwa na uwepo wa Wanyama wa aina mbalimbali wakiwemo Wanyama maarufu watano (Big Five). 








Share To:

JUSLINE

Post A Comment: