KORONGWE

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Basila Mwanukuzi ameahidi kuhakikisha maji yanafika kwenye shule ya Sekondari Mashewa ili kuwapunguzia kero ya maji wanafunzi wawapo masomoni.


Ahadi hiyo ameitoa alipozindua Bweni lenye uwezo wa kubeba wasichana 48 lililojengwa na Wananchi kwa msaada wa shirika la HakiElimu.


Mhe. Basila amesema jitihada wanazozifanya HakiElimu na wadau wengine zimechangia kuwapa fursa kubwa wasichana na Wilaya yake itaendela kushirikiana nao ili kuleta usawa katika safari ya Elimu kwa watoto wa Korogwe.


“Changamoto ni nyingi na mimi Kama mlivyosema kwenye risala nitaondoka na hii changamoto ya maji naichukua na nitaiwasilisha kwa injia wa maji ili shule pamoja na wananchi wawe wanufaika wa maji” alisema Basila Mwanukuzi.


Mkuu huyo wa Wilaya pia amesema imefika wakati sasa ambapo jitihada kubwa zilizofanywa kwa watoto wa kike pia zielekezwe kwa watoto wa kiume ambao nao wameanza kurudi nyuma kwa kile kinachoonekana upendeleo kwa wasichana.


“Sasa hivi wanawake tuna nguvu sana kiasi kwamba wanaume nao wanarudi nyuma, nafasi yenu wanaume ipo pale pale, nimeteta na Mkurugenzi wa HakiElimu hapa, nikamwambia kweli tunafanya mambo mengi kumwezesha msichana kwa sababu amepata changamoto kubwa, lakini tusisahau wavulana.


“kwa upendo huo huo ambao wasichana tunajengewa, pia hatuachi kuwatahmini na kuwasaidia watoto wa kiume, hawa wanaenda kuwa Baba, na tunaambiwa baba ndiye kichwa cha familia, kwa hiyo katika elimu lazima tujenge misingi bora pia ya kuwawezesha watoto wa kiume, katika misingi ya kimaadili na kiungozi, waweze kujiamini, wakati mwanawake anahamasika sana basi na wao wakahamasika ili jamii iwe na wananchi bora wenye uwezo wa kiakili kimwili na kiroho na waweze kutenda mema. Alisema dc Basila.


Naye Mkurugenzi wa HakiElimu Dkt. John Kalage amesema ufanisi wa utekelezwaji wa mradi huo uliofahamika kama AGE ulikuwa mahsus kwa watoto wa kike, ila umewapa changamoto ya namna ya kuhakikisha wanakuja na mikakati ambayo haitamwacha nyuma mtoto wa kiume kwenye safari ya Elimu.

Share To:

JUSLINE

Post A Comment: