Mwandishi wetu,Arusha


Zaidi ya sh,50  milioni zimetumika kugharamia chakula cha wanafunzi katika shule za msingi za Lengijape na Lemoot zilizopo  wilayani  Monduli mkoani Arusha.



Fedha za kugharamia chakula hicho  zimetolewa na shirika la maendeleo la Eclat Foundation lililopo Simanjiro mkoani Manyara .


Akizungumza wakati wa kukabidhi chakula hicho mkurugenzi wa shirika hilo,Peter Ole Toima amesema kwamba lengo kuu la kutoa chakula hicho ni kusaidia jamii ya wafugaji wa eneo hilo ambao wameshindwa kumudu gharama za michango ya chakula mashuleni kutokana na uhaba wa mvua.


Ole Toima alisema kwamba tatizo la uhaba wa mvua limepelekea wakazi wa maeneo hayo kukosa chakula na fedha za michango mashuleni hivyo wao kama shirika wameona waingilie kati kutatua changamoto hiyo.


"Wakazi wa eneo hili wanategemea mifugo na kilimo ambavyo katika siku za nyuma mvua hazijanyesha hivyo baadhi ya  wazazi wameshindwa kuchangia  fedha za chakula na watoto kushindwa kupata mahitaji yao" alisema Toima 


Hatahivyo,alisema kwamba mpango wa ugawaji wa chakula katika shule hizo ni wa dharula kutokana na mabadiliko ya tabia nchi huku ukiwa na malengo ya kuongeza idadi ya wanafunzi kuhudhuria masomo shuleni.


Naye afisa elimu msingi wa wilaya ya Monduli,Natadang'uaki Mollel alisema kwamba mpango huo wa chakula utasaidia kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule hizo kutokana na wanafunzi kuhudhuria kikamilifu masomo.


Mwenyekiti wa halmashauri ya Monduli,Isaack Kadogoo alisema kwamba asilimia kubwa ya mazao ya wakazi wa eneo hilo yameharibiwa na wanyama pori na hivyo kupelekea ukosefu wa chakula.


Mwenyekiti huyo alisema kwamba suala la chakula cha wanafunzi mashuleni ni eneo mojawapo ambalo wanelitilia mkazo na kuwaomba wadau wengine  kujitokeza kuunga mkono zoezi hilo.


Diwani wa viti maalumu wa tarafa ya Kisongo,Pauline Mollel alisema kwamba mpango huo utasaidia kupunguza utoro mashuleni kwa kuwa baadhi ya wanafunzi walishindwa kuhudhuria masomo kutokana na njaa.

Share To:

Post A Comment: