Mkuu wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Kalisti Lazaro (katikati) akihojiwa na waandishi wa habari mara baada ya kupokea baadhi ya mabomba yatakayojenga miradi minne ya maji wilayani Lushoto kwa fedha za UVIKO 19. Kulia ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga. (Picha na Yusuph Mussa)
Baadhi ya mabomba yatakayojenga miradi minne ya maji wilayani Lushoto kwa fedha za UVIKO 19. (Picha na Yusuph Mussa)
Baadhi ya mabomba yatakayojenga miradi minne ya maji wilayani Lushoto kwa fedha za UVIKO 19. (Picha na Yusuph Mussa)
Fuso likishusha baadhi ya mabomba yatakayojenga miradi minne ya maji wilayani Lushoto kwa fedha za UVIKO 19. (Picha na Yusuph Mussa)

Na Yusuph Mussa, Lushoto

Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga imepata fedha za UVIKO 19, ambapo miradi minne ya Bungoi, Kwesimu, Mbwei na Mayo itatekelezwa mwaka huu ili kuwaondolea kero ya maji wananchi.

Hayo yalisemwa Februari 13, 2021 na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Mijini na Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga kwenye hafla fupi ya Mkuu wa Wilaya hiyo Kalisti Lazaro kupokea mabomba yenye urefu wa kilomita 33.6 yakiwa yenye kipenyo tofauti kwa ajili ya miradi hiyo, iliyofanyika Ofisi za RUWASA Lushoto.

"Serikali imetupatia mabomba yenye urefu wa kilomita 33.6 kwa ajili ya utekekezaji wa miradi minne kupitia fedha za UVIKO 19. Miradi hiyo ni ule wa Bungoi ambao kutakuwa na ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lita 175,000, ujenzi wa chanzo cha maji, ujenzi wa vituo 15 vya kuchotea maji, uchimbaji wa mtaro mita 13,500, ulazaji wa mabomba ya kusafirisha maji mita 4,200 na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji mita 9,300, mradi wote ukigharimu sh. milioni 507.

"Ukarabati wa chanzo cha maji Kwesimu utagharimu sh. milioni 250, ambapo kazi zake ni ujenzi wa chanzo cha maji, ulazaji wa mabomba ya kusafirisha maji mita 2,800, uunganishaji wa bomba kwenye tanki na uchimbaji wa mtaro mita 2,800" alisema Sizinga.

Sizinga alisema mradi mwingine ni ule wa Mbwei, ambapo kazi zake ni ujenzi wa chanzo cha maji, ulazaji wa bomba la kusafirisha maji mita 1,500, uunganishaji wa bomba kwenye tenki, uchimbaji wa mtaro mita 8,800, ulazaji wa bomba, ujenzi wa tanki lita 90,000 na ujenzi wa vilula (DP), gharama yake ikiwa sh. milioni 280.

Mhandisi Sizinga alisema mradi mwingine ni Mradi wa Maji Mayo uliopo Halmashauri ya Bumbuli, ambao utagharimu sh. 497,960,800, na shughuli zitakazofanyika ni ujenzi wa chanzo cha maji, ulazaji wa bomba la kusafirisha maji mita 1,100, uunganishaji wa bomba kwenye tenki, uchimbaji mtaro mita 6,800, ulazaji wa bomba na ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lita 90,000.

Mkuu wa Wilaya, Lazaro, alimshukuru Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha za UVIKO 19 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. Alisema wilaya hiyo haina shida ya vyanzo vya maji, bali miundombinu ya maji, hivyo kwa kupeleka fedha hizo, wananchi wa Lushoto watapata maji safi na salama.

"Tunamshukuru Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa kutuletea fedha hizi za UVIKO 19, sasa ameonesha kuwajali wananchi wa Lushoto, na sasa tutapata maji kwa zaidi ya asilimia 70. Sisi wananchi wa Lushoto hatuna shida ya vyanzo vya maji, bali miundombinu yetu ya maji ndiyo chakavu, hasa katika mji wa Lushoto. Lakini kwa baadhi ya vijijini, miundombinu hiyo ilikuwa haijafika kabisa" alisema Lazaro.

MWISHO.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: