Mbunge wa Tanga Mjini na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe Ummy Mwalimu  leo tarehe 7/01/2022 amekagua ujenzi wa shule mpya ya Sekondari iliyopo Saruji, Kata ya Maweni Jijini Tanga ambapo  madarasa 14  yamejengwa kwa pesa za UVIKO kiasi cha  shilingi milioni 280. Mhe Ummy ameridhishwa na ujenzi huo. Aidha amewapongeza Viongozi na Watendaji wa Jiji la Tanga kwa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati. 


Pia amefurahishwa na hatua ya Jiji la Tanga kutumia mapato yake ya ndani kujenga matundu ya vyoo 12 kwa ajili ya wanafunzi na maabara 1 ya masomo ya Sayansi. 


Mhe Ummy amewataka  Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuiga mfano wa Jiji la Tanga na kuhakikisha wanatumia mapato ya ndani kujenga matundu ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi ili kuendana na ongezeko la madarasa ya Samia yaliyojengwa kwa fedha za UVIKO. 


Wakiongea kabla ya kumkaribisha Mhe Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe Hashim Mgandilwa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Maweni Ndugu Mpokigwe Anyitike wamempongeza Rais Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa madarasa 54 kwa mpigo kwa ajili ya wanafunzi wa Jiji la Tanga jambo ambalo halijahi kutokea! Pia wamemshukuru Mhe. Ummy kwa kazi nzuri ya kumsaidia Rais Samia na kazi nzuri anazozifanya kutatua kero za wana Tanga. Aidha wameomba Shule hiyo iwe ya Wasichana na iitwe Ummy Mwalimu Girls Secondary School.


Katika ziara hiyo, Mhe Ummy aliambatana na Katibu wa CCM Wilaya ya Tanga Ndg. Twalibu Bellege, Diwani Viti Maalum, Mhe Mariamu Ng'azi na wakuu wa idara na Watumishi wa Halmashauri wa Jiji la Tanga.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: