Na,Jusline Marco;Arusha



Zaidi ya watu 300 wapatiwa mafunzo kwa mwaka wa fedha 2021 ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya Sheria namba 7 ya Nguvu za Atomiki Tanzania ikielekeza Tume ya Nguvu za Atomiki kutoa mafunzo kwa watumiaji wa vyanzo vya mionzi nchini.



Mkuu wa Utafiti na Mafunzo kutoka TAEC ,Shovi Sawe amesema hayo wakati wa utoaji wa vyeti kwa wahitimu wa mafunzo ya Usalama wa vyanzo vya mionzi vinavyotumika katika ukaguzi wa mizigo.



Shovi amesema mafunzo hayo ambayo yametolewa kwa makundi 3 likiwemo kundi la watu kutoka katika Baraza la wawakilishi Zanzibar, yamelenga kuwajengea uwezo ili waweze kuelewa namna salama ya kufanyiakazi vyanzo hivyo na kuweza kuwa salama.



Aidha katika mafunzo hayo washiriki wameelekezwa namna nzuri ambayo wataitumia baada ya vyanzo vya mionzi kuisha ili viwe salama ikiwa ni pamoja na kurudisha vyanzo hivyo Tume ya Atomiki Tanzania kwa ajili ya uhifadhi kwenye stoo ya kitaifa.



Amesema suala la utii wa sheria katika mionzi ni muhimu kwani mionzi ni moja ya vitu ambavyo vinamanufaa makubwa katika jamii kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii lakini isipotumika vizuri ni mibaya hivyo mafunzo hayo yamekusudia kutoa njia ambayo itatumika ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi,raia na mazingira unakuwepo.



Awali akifunga mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAEC Njiro Jijini Arusha,Dkt.Remegius Kawala ameyataka makundi hayo kuchangamkia fursa na huduma ambazo zipo TAEC kwa lengo la kujali afya zao sambamba na utii wa sheria zilizopo.




Dkt.Remegius mesema jambo la muhimu la kuzingatia ni kujua usalama wa mazingira ambao mtu anafanyiakazi kwa kufahamu viwango vya mashine aliyonayo mtu ili kujua kama viwango vya mionzi vimezidi kwani usalama wakati mwingine hubadilika ambapo amesema kutokana na  ukubwa wa taasisi ya TAEC wameona ni wajibu wao wawe na vifaa vyao kwa ajili ya kuendesha mafunzo.




"Kuanzia mafunzo yajayo mambo yote tutakuwa tunamalizia hapa hapa,wataalamu wako hapa kwa wale ambao watapenda kwenda advance zaidi tutawaruhusu mchomoe baadhi ya vifaa ili muweze kipata mafunzo alisia ya vitendo."alisisitiza Dkt.Remegius




"Hatusemi kana kwamba teknolojia ya mionzi ina madhara,lakini kitu chochote kina madhara endapo utakiuka kukitumia,kila kitu ambacho chenye matumizi mazuri ukikikiuka kina kuwa na matumizi ambayo yanaweza kukuletea matatizo mengine."




Sambamba na hayo amewataka wote waliopata mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri kwa wengine kwa kuwashawishi ili waweze kupata mafunzo hayo kwa manufaa yao kwani lengo la TAEC ni wafanyakazi wawe na uelewa wa masuala ya mionzi.




Ameongeza kuwa mafunzo yanayotolewa yapo kwa mujibu wa sheria namba 7 ya Nguvu za Atomiki ambayo inawataka kutoa mafunzo kwa wataalamu wenye uelewa wa teknolojia hiyo na usalama wake ambapo amesema utii kwenye sheria utamsaidia mtu kujua eneo,mashine na jengo lake lilivyo na ni vyema mtu akajali mazingira yaliyopo na ya mwingine.

Share To:

Post A Comment: