▪️ Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba yazinduliwa rasmi


▪️ Wajumbe wa Bodi watakiwa kushauri kuhusu Sheria ya Bodi Na. 6 ya mwaka 1975


Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Maktaba Mtandao ili  kuongeza wigo wa upatikanaji huduma za maktaba kutokana na ongezeko la idadi ya watumiaji wa huduma hiyo nchini.


Hayo yamesemwa leo Januari 3, 2022 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (Mb) wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (BOHUMATA) ambapo amesema fedha hizo ni sehemu ya Shilingi bilioni 10.5 za bajeti ya maendeleo ya Bodi hiyo zilizotolewa na Serikali katika mwaka wa fedha 2021/22.


Aidha ameitaka Bodi hiyo kuhakikisha katika utafutaji wa machapisho na vitabu izingatie kupata vitabu vinavyolenga kukuza ujuzi, maarifa na stadi mbalimbali kwa Watanzania wote wakiwemo wenye mahitaji maalum.


"Nitoe rai kwa Bodi kuhakikisha mnatafuta machapisho na vitabu  vinavyolenga kukuza ujuzi, maarifa na stadi mbalimbali. Tunataka maktaba iwe kwa Watanzania wote yaani watoto, wajasiriamali, walemavu wa aina mbalimbali, wakulima, wafugaji, watafiti wote waweze kupata huduma hii muhimu," amesisitiza Waziri Ndalichako.

Share To:

Post A Comment: