MKURUGENZI wa Kampuni ya Usafiri ya Tashirif Salum Said akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake |
ABIRIA
waliokuwa wakisafiri kwenda katika mikoa mingine kutokea kituo kikuu
cha mabasi kilichopo Kange Jijini Tanga, walilazimika kuondoka saa moja
asubuhi badala ya saa kumi na mbili, baada ya kampuni ya mabasi ya
Tashiriff kuyazuia katika lango kuu la kutokea.
Kadhia
hiyo ya abiria kuchelewa kuondoka ilitokea leo saa 12:00 asubuhi
katika kituo cha mabasi cha Kange, baada ya basi la Tashiriff lenye
namba za usajili T 369 DYD lililokuwa likitaka kutoka kwenda Masasi
mkoani Mtwara kuzuiwa na maafisa wa LATRA wakidai basi hilo muda wake ni
saa 12:30 na siyo muda huo wa saa 12:00 asubuhi.
Baada
ya kuzuiwa basi hilo halikuondoka katika lango kuu la kutokea licha ya
kutakiwa kuondoka kupisha magari mengine yatoke lakini halikuondoka na
badala yake Mkurugenzi wa kampuni hiyo aliyefahamika kwa jina la Salim
Hamoud Said kuweka gari lake dogo kuzuia magari mengine.
"Tajiri
wa Tashiriff alifika na gari lake dogo pia alifunga geti, huku
akilalamika kwamba LATRA inafanya upendeleo wa ratiba za kusafiri kwa
mabasi mengine," alisema abiria mmoja aliyekuwa akisafiri kwenda
Shinyanga na Kapricorn.
Askari
wa usalama barabarani waliokuwa katika kituo kikuu hicho cha mabasi,
hawakufanya chochote licha ya abiria kulalamika kuchelewa kuondoka
katika muda wa saa 12:00 asubuhi.
Polisi
wengine walifika na kumchukua mkurugenzi huyo wa Tashiriff saa moja
asubuhi wakati ambao ndiyo mabasi karibu yote yaliyokuwa yakisafiri
kwenda mikao mingine yaliondoka baada ya basi hilo kuondolewa muda huo.
Akizungumza
baadaye baada ya kutoka kituoni saa 13:00 mchana jana, alisema aliamua
kufanya hicho kama njia mojawapo ya kufikisha kilio chake kwa serikali
kuhusu hatua ya LATRA kushindwa kuwapa ratiba ya muda wa saa 12:00
asubuhi kwenda Mtwara.
"Leo
tumefanya mgomo kwasababu siyo haki tunayofanyiwa na LATRA, sisi basi
letu linakwenda kilomita 950 halafu hawataki kutupa ratiba ya saa 12:00
kamili kama mabasi mengine kwanini?," alisema mmiliki huyo.
Mmiliki
huyo alisema mara kadhaa ameomba ratiba ya saa 12:00 amepewa lakini
baada ya kuifanyia kazi wiki moja ananyang'anya karibu mara nne
alishapewa na hajui ni sababu gani amekuwa anasumbuliwa.
"LATRA
wamenipa ratiba hii Januari 6 mwaka huu ya saa 12:00 leo wamenizuia
nisiondoke muda huu wanataka niendelee na ratiba ya saa 12:30 na ndiyo
maana tumeamua kugoma pale kituoni," alisema na kuitaka serikali
ifuatilie kuona ratiba za mabasi Tanga kuna nini?.
Hata
hivyo, alisema basi yake ya kwenda Masasi mkoani Mtwara iliondoka saa
3:00 asubuhi hatua ambayo inasababisha abiria kuteseka njiani kwa
kusafiri muda mrefu njiani.
Kwa
upande wa wamiliki wa mabasi mengine wakizungumzia kadhia hiyo walisema
kwamba inatakiwa kukomeshwa na serikali kwasababu haiwezekani mmiliki
mmoja anaamua kuzuia mabasi mengine halafu hachukuliwi hatua.
Wakala
wa kampuni ya mabasi ya Simba mtoto katika kituo hicho Saleh Issa
alisema kwamba baada ya kampuni ya Tashiriff kufunga lango la kutokea
walilazimika kutumia mlango wa kuingilia ili waweze kusafiri baada ya
abiria wao kuanza kulalamika wakielezea sababu ya kwanini wametaka
kuondoka muda huo wa asubuhi.
Wakala
huyo alisema walikuwa na abiria waliokuwa na tiketi za boti za kwenda
Zanzibar saa 12:00 mchana hivyo wanavyozidi kuchelewa nani atawalipa
gharama za kukosa safari ambayo tayari waliiandaa.
"Kiukweli
tulilazimika kupita No entry tena ilikuwa saa 7:00 asubuhi maana mule
ndani tulikuwa na abiria wanaokwenda Bandarini, uwanja wa ndege na
wengine walikuwa na ahadi na madaktari wa Muhimbili," alisema Saleh na
kuiomba serikali ilitazame suala hili ili lisijirudie tena.
Kamanda
wa polisi wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Tanga Mrakibu wa
Polisi (SP) Leopold Fungu alipoulizwa kuhusu suala hilo kwanza alisema
linatakiwa kuzungumzwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Vyombo vya nchi kavu
(LATRA) na si yeye.
"Hilo
tatizo la asubuhi na mabasi kuzuiwa nadhani watafute LATRA, sisi
tulimkamata mmiliki wa Tashiriff kisha tukamuachia tulimshitaki kwa kosa
la Obstruction," alisema Kamanda Fungu.
Akizungumzia
suala hilo kwa njia ya simu, Meneja wa LATRA mkoani Tanga Kenedy
Nyakabondo alipouliza sababu za kwanini wasiwape ratiba ya saa 12:00
kampuni hiyo ya Tashiriff, alisema atatoa majibu baada ya wiki tatu
kwakuwa hayupo Tanga hivyo hadi arudi.
Post A Comment: