Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki ( wapili kulia) akimsikiliza mmoja wa Wafugaji wa Kijiji cha Kiwege, Mkoani Morogoro muda mfupi baada ya kumaliza kikao na Wafugaji wa Kijiji hicho jana.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akiteta Jambo na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando wakati wa kikao baina ya Waziri Ndaki na Wafugaji wa Kijiji cha Kiwege, Kata ya Ngerengere, mkoani Morogoro jana.
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akiagana na  Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martine Shigela (katikati) muda mfupi baada kumaliza mazungumzo yao katika Ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa mapema leo Disemba 7, 2021. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Amosy Zephania.


Na Mbaraka Kambona, Morogoro.


WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inawajali Wafugaji na ndio maana  inaendelea  kufanya kila linalowezekana  kuwawezesha wafanye shughuli zao kwa tija.

Waziri Ndaki aliyasema hayo jana katika ziara yake mkoani Morogoro na Pwani ambayo lengo lake lilikuwa kutembelea maeneo yaliyokumbwa na ukame na kuathiri ustawi wa mifugo nchini.

"Rais wetu anawajali wafugaji na ndio maana anafanya kila linalowezekana ikiwemo kuipatia fedha Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili iweze kuwahudumia Wafugaji waweze kufanya shughuli zao kwa tija," alisema Ndaki.

Alisema katika kuhakikisha Wafugaji wanaendelea kufanya shughuli zao kwa ufanisi, Rais Samia amezielekeza Wizara nane (8) chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuvibakisha katika maeneo yake Vijiji 920 ambavyo vilikuwa na migogoro.

"Mhe. Rais ameilekeza Wizara ya Ardhi  kuweka utaratibu mzuri wa namna ya kuwabakisha wale wanaoishi katika Vijiji hivyo ambapo robo tatu ya maeneo yote ya Vijiji hivyo wanakaa wafugaji," alifafanua.

Aidha, Waziri Ndaki aliongeza kuwa Mhe. Rais Samia ameridhia kwamba baadhi ya Vijiji ambavyo maeneo yake yalichukuliwa na kufanywa eneo huru la uwindaji yarudishwe kwa wanakijiji ili wayatumie kwa matumizi mengine.

"Nipende kuwahakikishia Wafugaji kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumeanza utaratibu wa kuyarasimisha kisheria kwa kuyatangaza kwenye  gazeti la Serikali maeneo yote yaliyotengwa  kwa ajili ya Wafugaji kwenye Wilaya zenu," alibainisha.

Pia, Waziri Ndaki aliwatahadharisha Wafugaji hao kutoingia kiholela katika vyanzo vya maeneo ya maji, maeneo tengefu kwasababu yanalindwa kisheria na  hivyo ni makosa kuingia mifugo yao.

Awali, Mmoja wa Wafugaji kutoka Kijiji cha Kiwege, Kata ya Ngerengere, mkoani Morogoro, Seif Lekake alimueleza Waziri Ndaki kuwa ukosefu wa miundo mbinu na ufinyu wa maeneo waliyonayo kwa ajili ya kufugia unachangia mifugo kuingia katika maeneo ambayo sio ya ufugaji.

"Mhe. Waziri tunahitaji msaada wako ili haya maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya Wafugaji yatafutiwe namna ya kupimwa ili yaweze kulindwa kisheria yasiendelee kumegwa kwa sababu baada ya muda yatapotea na Wafugaji wataendelea kutangatanga," alisema Lekake.

Kaimu Katibu wa Chama cha Wafugaji Wilayani Kibaha, George Mfuko alisema kuwa pamoja na ukame uliyoikumba nchi, matatizo makubwa wanayokumbana nayo Wafugaji ni maeneo ya kufugia na maji ya kunyweshea mifugo na hivyo alimuomba Waziri aweze kuwawekea miundombinu ya maji ili mifugo iwe na uhakika wa maji.

"Katika kipindi hiki cha ukame imefika mahali unanunua dumu la maji la lita mia mbili  kwa ajili ya kuwapa mifugo, hili limekuwa ni changamoto kubwa sana kipindi hiki," alisema Mfuko.

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: