Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akionesha muelekeo wa Mpaka wa Kimataifa baina ya Tanzania na Kenya katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara tarehe 21 Dsemba 2021 wakati wa ziara yake ya kukagua kazi ya uimarishaji mpaka huo.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akielekea kukagua alama za Mpaka wa Kimataifa baina ya Tanzania na Kenya eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara tarehe 21 Dsemba 2021.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipiga hatua kujiridhisha umbali wa alama moja ya mpaka na nyingine wakati wa ziara yake ya kukagua uimarishaji Mpaka wa Kimataifa baina ya Tanzania na Kenya katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara tarehe 21 Dsemba 2021.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na dereva kutoka idara ya Upimaji nchini Kenya Bi. Habiba Huka (Kushoto) wakati wa ziara yake ya kukagua alama za uimarishaji mpaka kati ya Tanzania na Kenya kwenye eneo la Serengeti mkoani Mara tarehe 21 Dsemba 2021. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiwa katika picha ya pamoja na timu ya Kenya inayoshiriki kazi ya uimarishaji mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya wakati wa ziara yake ya kukagua uimarishaji mpaka wa nchi hizo eneo la Serengeti mkoani Mara tarehe 21 Dsemba 2021.

*****************

Na Munir Shemweta, WANMM TARIME

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekagua uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya Tanzania na Kenya katika eneo la hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara na kupongeza wapima wa nchi hizo mbili kwa kufanikisha kuweka alama 205.

Aidha, Waziri Lukuvi aliwashukuru marais wa Tanzania na Kenya kwa kukubaliana kuendelea na kazi ya uimarishaji mpaka huo wa kimataifa kwenye eneo la hifadhi ya Taifa ya Mbuga ya Serengeti na Masai Mara kwa upande wa Kenya ambapo uimarishaji wake ulisimama kwa muda.

‘’Kwa muda mfupi timu za nchi hizo mbili zimeweza kuweka alama 205 katika eneo hili, kazi ilianza 2018 tulipofika eneo la hifadhi tulisiamama kidogo na uendelezaji huu unaofanyika umechangiwa na ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan kule nchini Kenya kuzungumza na mwenzake Uhuru Kenyata na kukubaliana na ndiyo maana wapima wamendelea na kazi hiyo’’ . alisema Lukuvi

Akiwa katika eneo la Serengeti tarehe 21 Desemba 2021 katika ziara ya kukagua uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya, Waziri Lukuvi alisema, anaamini sasa nchi hizo mbili zinaenda kumaliza kuweka alama kwenye mpaka mzima unaofikia kilomita 758 ambapo kwa sasa zimefikiwa kilomita 232 na kuahidi zote kumalizwa.

Akigeukia kuhusu eneo la ukingo wa mpaka (Buffer Zone) Waziri Lukuvi alisema, kwa sasa ni vyema utengenezaji barabara ukazingatia eneo la mita tano aliyoieleza kuwa ni muafaka wa nchi hizo mbili na kuongeza kuwa, mazungumzo bado yanaendelea kuona kama ipo haja ya eneo hilo kuongezwa.

‘’Serikali itaendelea kusaidia ili kazi hii ya uimarishaji mipaka ya Kimataifa iende vizuri na uwekaji alama hizi siyo uadui bali ni kuwa na mipaka inayoonekana itkayoondoa hofu. Kama mtu akitaka kufanya uovu asisingizie kama hajui mpaka na alama tutaweka kote hata majini’’. Alisema Lukuvi.

Mkurugenzi wa Upimani na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansour .alisema, kazi mbalimbali zimefanyika wakati wa uimarishaji mpaka mpaka huo zikiwemo utoaji elimu, kuanisha sehemu ya kujenga, kujenga alama za mpaka pamoja na kukusanya taarifa za kijiografia.

Mpima kutoka Idara ya Upimaji nchini Kenya Ibrayan Sabwa alieleza kuwa, katika kipindi chote cha kazi ya uimarishaji mpaka eneo la hifadhi ya Taifa ya Serengeti na ile ya Masai Mara kwa upande wa Kenya wamekuwa na ushirikiano mzuri baina ya timu za nchi hizo na kubainisha kuwa na hakukuwa na shida yoyote wakati wa kazi hiyo.

‘’Tumekuwa tukiendelea vizuri, na kazi imeenda vizuri sana, watanzania wamekuwa wakishirikiana na sisi vizuri hawakuwa na shida yoyote na nina imani kazi itakamilika vizuri. Watanzania ni marafiki zetu na wao ni marafiki zetu’’ alisema Sabwa.

Mapngo kazi wa mwaka wa fedha 2021/2022 kuhusiana na uimarishaji mipaka wa Tanzania na Kenya ni kukamilisha awamu ya I ya Km 238 kwa kukamilisha kipande cha hifadhi cha Km 60 na eneo la Natron la Km 23 pamoja na kuimarisha awamu ya II yenye jumla ya kilomita 110 ya mpaka kutoka Ziwa Natron hadi Namanga katika wilaya ya Longido.

Mpaka wa Tanzania na Kenya una urefu wa nchi kavu wa Km 758 uliowekwa kwa makubaliano ya wakoloni wa Kijerumani na Kiingereza mwaka 1893 chini ya mkataba wa Anglo-Germany Agreement na Protocal kukubalika mwaka 1906.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: