Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) wameaswa kutumia fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini kujiajiri badala ya kusubiri ajira rasmi.


Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa TAHLISO 2021/2022 uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya African Dreams uliopo jijini Dodoma. 


Aidha, Waziri Biteko ametoa Wito kwa Jumuiya ya TAHLISO kujifunza kwa bidii na kutafuta maarifa na uzoefu mpya ili siku moja wakiwa viongozi waweze kubadilisha maisha ya watu.


“Watu hawashindani kwa kufahamiana wala watu hawashindani kwa kujuana lakini watu wanashindana kwa uwezo wao, hivyo niwaombe mtumie fursa hii mliyoipata ya kusoma elimu ya juu kupambana ili mpate uwezo wa kupambanua mambo, dhana za kujuana hizo zilipendwa,” amesema Waziri Biteko.


Pia, Waziri Biteko amewashauri wanafunzi hao kujijengea uwezo wa kupambanua mambo na kuyaelewa na pia kusoma kwa bidii ili mwisho wa siku waweze kuingia kwenye soko la ushindani.


Waziri Biteko amesema Mlezi wa TAHLISO ambaye ndiyo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan  anawaamini na ametoa msukumo mkubwa na kipaumbele kwa viongozi wa Taasisi hiyo .


“Ukiwa unasoma darasani usiwaze GPA peke yake, waza na ujiulize ni kitu gani utakiacha baada ya maisha yako ya shule na baada ya maisha yako hapa duniani,” amesema Waziri Biteko.


Pia, Waziri Biteko amewapongeza TAHLISO kwa kuchagua uongozi kwa kuzingatia usawa wa jinsia baada ya kuona ulinganifu wa jinsia zote kwenye nafasi za uongozi.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAHLISO Frank Nkinda amemuomba Waziri Biteko kufikisha salamu za TAHLISO kwa Mlezi wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini na kuwaunga mkono katika harakati zao za kutafuta elimu na maarifa. 


Mkutano huo wa siku mbili umebebwa na Kauli Mbiu isemayo "Miaka 60 ya Uhuru na Mageuzi ya Elimu ya Juu Nchini."    

Share To:

Post A Comment: