Afisa Viwango Bi Zena Issa (TBS) akitoa mafunzo ya sumukuvu kwa wafanyabiashara, wasafirishaji na wasindikaji wa mahindi na karanga pamoja na bidhaa zake wilayani Kilosa, Morogoro. TBS imeendesha mafunzo hayo kupitia Mradi wa Kitaifa wa Kudhibiti Sumukuvu kwa wilaya ya Kiteto mkoa wa Manyara,Kongwa mkoa wa Dodoma ,Gairo na Kilosa mkoa wa Morogoro.


****************

Na Mwandishi Wetu, Kilosa

WAFANYABIASHARA, wasafirishaji na wasindikaji wa mazao ya mahindi na karanga pamoja na bidhaa zake zaidi ya 500 katika wilaya za Kiteto mkoa wa Manyara, Kongwa mkoa wa Dodoma, Gairo na Kilosa mkoa wa Morogoro wamepatiwa mafunzo kupitia Mradi wa Kitaifa wa Kudhibiti Sumukuvu "Tanzania Initiative for Preventing Aflatoxin Contamination (TANIPAC).

Mafunzo hayo yalianza kutolewa kuanzia tarehe 24 Novemba 2021 hadi tarehe 8 Desemba 2021 katika wilaya nne ambazo zipo katika mikoa mitatu nchini kwa lengo la kudhibiti sumukuvu ili kulinda afya za binadamu, kuwezesha biashara ya mazao ya mahindi na karanga, kulinda afya za mifugo na kuwezesha utoshelevu wa chakula salama.

Akizungumza wilayani Kilosa mkoani Morogoro wakati wa kufungua mafunzo hayo leo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania TBS, Jabir Saleh Abdi, alisema Serikali kupitia TBS ilianza kutoa mafunzo hayo kupitia Mradi wa Kitaifa wa Kudhibiti Sumukuvu wilayani Kiteto mkoani Manyara Novemba 24, mwaka huu, ambapo mafunzo hayo yameweza kuwajengea uelewa mkubwa walengwa.

Kwa mujibu wa Abdi mradi huo upo chini ya Wizara ya Kilimo na TBS imekabidhiwa jukumu la kutoa mafunzo hayo.

Alisema mafunzo hayo yanategemewa kuendelea kutolewa katika Wilaya za Kondoa, Chemba, Bahi, Babati. Wilaya nyingine ni Namtumbo, Newala, Nanyumbu, Nzega, Urambo, Kibondo, Kasulu, Buchosa, Bukombe na Itilima. Kuhusu mikoa ambapo mafunzo hayo yatatolewa, Abdi alisema ni Dodoma, Manyara, Ruvuma, Mtwara, Tabora, Kigoma, Mwanza, Geita, Simiyu na Morogoro.

Abdi alitaja faida za mafunzo kuwa yamelenga kulinda afya za binadamu, kuwezesha biashara ya mazao ya mahindi na karanga, kulinda afya za mifugo na kuwezesha utoshelevu wa chakula salama.

Alitaja faida nyingine kuwa kuhimili ushindani katika masoko ya ndani, kikanda na nje ya nchi.

Abdi amewasihi washiriki kuwa mabalozi wazuri wa mafunzo hayo na kuzingatia mambo muhimu yanayoshauriwa na wataalam ili kudhibiti sumukuvu.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: